Maana
na makusudi ya kujaribiwa
Jaribu linasemekana kuwa ni mtaji wa kuinua imani ya
mtu anayejaribiwa, lakini binafsi ninapenda kuirekebisha sentensi hii. Jaribu
ni mtaji wa kuinua imani ya anayeshinda jaribu; kama umejaribiwa na jaribu
likakuangusha, siyo sahihi kusema jaribu hilo lililokuangusha lilikuwa mtaji wa
kuinua imani yako. Imani ipi? Kama umeshindwa kuitetea imani yako na
kuangushwa, jaribu halikuwa mtaji kwako.
Jaribu huja na makusudi mawili; moja, ni
kumuimarisha kiroho na kuinua imani ya anayejaribiwa na kushinda jaribu. Pili,
ni kumuangusha mtakatifu na kuharibu uhusiano wake na Mungu. Na mara nyingine
jaribu au teso huwa ni kiboko cha Mungu cha kulirudi kanisa lake. Ninaposema
kanisa ninamaanisha Mkristo.
Kuinua imani ya Mkristo. Nikupe mfano kwanza, kuna
hekima ya Kimungu na hekima ya kibinadamu.
Hekima ya Kimungu hupewa mtu yoyote pasipo kujari umri, na hii huletwa
na Yesu Kristo mwenyewe. Na hekima ya kibinadamu huja kutokana na uzoefu wa
muda mrefu alionao mtu katika jambo fulani, na hekima hii wanayo wazee. Na
imani ndivyo ilivyo, ili ikue ni lazima ipitishwe katika kujaribiwa, ipitishwe
katika vitu ambavyo sayansi na akili ya kibinadamu haviwezekani. Ukiisha pita
hapo kwa msaada wa Mungu kwa jina la Yesu Kristo ndipo imani yako inapokuwa.
Ndipo unapozidisha imani na uhusiano wako na Mungu kupitia Yesu Kristo (Yohana
11:3-4, 14-15 na 1 Petro 1:6-7)
Kumuangusha mtakatifu. Hili ni jaribu linalosababishwa
na shetani moja kwa moja, na makusudi yake huwa ni kumuangusha mtakatifu ili
kuharibu na kufuta kabisa uhusiano wake na Mungu. Kwa mfano, Ayubu hakujaribiwa
ili kuinua imani yake au kurudiwa na Mungu, alijaribiwa ili amkufuru Mungu, kwa
Kiswahili chepesi ni ili avunje uhusiano wake na Mungu. Kwa hiyo kuna wakati
shetani huwajaribu Wakristo ili awafarakanishe na Mungu (Yohana 2:10, Ayubu
2:4-5)
Kurudiwa na Mungu. Hapa naomba nieleweke, hili kwa
upande mmoja siyo jaribu na kwa upande mwingine ni jaribu. Nina maana gani; kwa
upande wa Mungu ni kiboko cha kulirudi kanisa lake kama ilivyo kwa mzazi
anapomuadhibu mtoto aliyekosea. Kwa upande wa Mkristo, analiona kama jaribu. Na
hili hutupata ikiwa tumekengeuka na kuiacha njia ya haki, tumemkosea Mungu. Na
tukitubu na kuirudia njia ya haki, utaona mateso yote yanaondoka pia (Mithali
3:11-12, Ayubu 5:17)
Nini
cha kufanya uwapo katika jaribu
Kuna makosa makubwa mawili ambayo Wakristo wengi
tunayafanya tuwapo katika majaribu. Na makosa haya ndiyo yanayogharimu uhusiano
wetu na kutufarakanisha na Mungu. Makosa hayo ndiyo yanayofanya tunaangushwa na
majaribu.
Kosa la kwanza; tunatumia akili zetu kutafuta
ufumbuzi wa jinsi gani tutavuka jaribu tunalopitia kwa ushindi na kumuacha
Mungu kando ambayo ndiye msaada wetu. Hapa ni lazima uelewe, Mungu pekee ndiye
anayetushindia majaribu, kwa akili zetu na nguvu zetu na maarifa yetu hatuwezi
kamwe kujinasua katika majaribu. Uwapo katika jaribu ni lazima umkabidhi Mungu
njia zako na jaribu lako, Yeye ndiye ushindi wako kwa Jina la Yesu Kristo (2
Petro 2:9, Zaburi 37:5)
Kosa la pili; kuwaangalia wanadamu wanafanya nini na
wanasema nini tunapopita katika jaribu hasa wapendwa au wakristo wenzetu. Kitu
tunachojisahau hapa ni kwamba tunategemea wingi wa marafiki tunaokuwa nao
wakati wa furaha ndio hao hao tutakao kuwa nao wakati wa majaribu, sivyo! Uwapo
katika shida au jaribu kama kuna mkristo mwenzako atabaki na wewe hiyo ni neema
tu ya Mungu, lakini wengi kama siyo wote watakuacha peke yako.
Unajua kwa nini watakuacha peke yako? Jaribu siyo
lao ni lako, anayepaswa kushinda siyo weo ni wewe. Kwa hiyo ni lazima upite
peke yako ili ushinde peke yako na tuzo ya ushindi utapata peke yako. Hupaswi
kuwaangalia wapendwa na hupaswi kulalamika iwapo watakuacha upite katika jaribu
peke yako.
Hebu tuangalie mfano; kuna wakati Yesu Kristo
alizuiliwa na Wasamaria kuingia katika kijiji chao, Yakobo na Yohana
walichukizwa na jambo hilo na wakataka kuagiza moto kutoka mbinguni ili
kuwaangamiza Wasamaria wale lakini Yesu Kristo aliwazuia (Luka Mtakatifu 9:51-56)
Ilipofika wakati Yesu Kristo anakikabiri kikombe cha
mateso, baada ya kuila pasaka aliwachukua wanafunzi wake hadi bustani ya
Gethsemane na akawachukua Petro, Yakobo na Yohana kwa ukaribu zaidi. Akawaambia
Roho yangu ina huzuni kiasi cha kufa, kaeni hapa mkeshe pamoja nami (muombe
pamoja nami), lakini wanafunzi hawa walipofika sehemu hii walilala wakamuacha
Yesu Kristo apambane mwenyewe. Kwa sababu hawakua na sehemu ya kukinywea
kikombe cha mateso cha Yesu Kristo (Mathayo Mtakatifu 26:36-40)
Kwa hiyo ninataka utambue kuwa uwapo katika jaribu
hupaswi kutumia akili, ufahamu, elimu na nguvu zako kujinasua kutoka katika
jaribu. Mruhusu Mungu akuvushe mwenyewe kwa utukufu wake kwa jina la Yesu
Kristo. Pia ni lazima wapendwa au wakristo wenzako wakuache ili uvuke wewe
mwenyewe kwa sababu unayejaribiwa ni wewe na siyo wao.
Namna
ya kupita katika jaribu ili upate ushindi wa heshima
Hapa ndipo penye kiini cha somo hili, namna
unavyopita katika jaribu ndivyo kunaamua namna na aina ya ushindi utakao upata.
Ukipita kwa akili zako utapata matokeo yanayolingana na akili yako, na hata
ukishinda hutapata ushindi wa heshima wenye utukufu wa Mungu. Kwa mfano wapo
mabinti wawili wanatafuta kazi, mmoja akatumia mwili wake (rushwa ya ngono) na
mwingine akamtumaini na kumtegemea Mungu, wote wanaweza kupata kazi, lakini
furaha ya kupata kazi na utukufu wa kazi utatofautiana na hata muda wa kudumu
katika kazi utatofautiana pia.
Unapopita katika jaribu, ni lazima uzingatie mambo
yafuatayo ili Mungu akupiganie na upate ushindi wenye sifa na utukufu kwa
Mungu, ushindi wenye taji safi kwa imani na ushuhuda wako.
Utii
kwa sauti ya Mungu
Unapokuwa na jaribu shetani huongea mara nyingi kwa
sauti nyingi, lakini Mungu huongea mara chache sana kwa sauti moja tu. Ni
lazima ukubali kuisikiliza, kuitambua na kuitii sauti ya Mungu, huo ndio
ushindi wako.
Yoshua 6:3-4. “Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote
wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita. Na makuhani saba
watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na
siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao.”
Kabla ya kufika katika mji wa Yeriko, Israeli
walipigana vita vingi na kama ni ujuzi wa vita basi walikuwa nao. Wangeweza
kuingia Yeriko pasipo kumshirikisha Mungu kwa sababu vita nyingi walizopigana
walishinda, walikuwa na kila sababu ya kujiamini. Lakini waliamua kumshirikisha
Mungu, na Mungu aliposema nao walimsikiliza na kutii sauti yake.
Watu wengi tunachokosea ni kwamba tunaomba msaada wa
Mungu na wakati tunasikiliza sauti nyingine tofauti na sauti ya Mungu. Mungu
anapotupa majibu, tunafuata na kutii sauti nyingine na siyo sauti ya Mungu, na
hapa ndipo tunajipata tumeangamizwa.
Kwa kutii maelekezo ya Mungu, Israeli walipata ushindi
wa kuuingia mji wa Yeriko kwani Mungu alifanya vita kwa ajili yao (Yoshua
6:15-16, 20).
Na wewe ukiamua kuisikiliza sauti ya Mungu na kutii
kufuata maelekezo yake, hakika ushindi utakuwa upande wako kwani Mungu mwenyewe
atapigana na adui zako kwa ajili yako.
Uwe
na imani, Mungu atatenda
Mungu ni Mungu wa ahadi, anatenda jambo kulingana na
ahadi iliyopo ndani ya neno lake. Pale tunapoona hakuna njia, kiza kinene
mbele, hatuna msaada ndipo Mungu hufanya njia hapo (Isaya 43:16).
Unapokuwa katika jaribu, kadri siku zinavyoongezeka
ndivyo unapaswa kuzidisha imani yako kwa Mungu. Na kama ulikuwa ukimuomba Mungu
mara moja kwa siku, ongeza maombi zaidi ikiwezekana hata mara tano kwa siku.
Ipo siri katika kufanya hivi, kwanza unamfanya Mungu aoneimani yako kwake
inakuwa na nia yako thabiti ya kuhitaji msaada wake. Pili, ni njia ya
kumdhohofisha shetani na kumfanya ashindwe vita na kukuachilia mara moja.
Ninakuhakikishia, kwa kufanya hivi ni lazima Mungu
atakuokoa katika jaribu lako kwa ushindi mkubwa na haraka iwezekanavyo.
Tunza
utakatifu
2 Petro 2:9. “basi, Bwana ajua kuwaokoa watauwa na
majaribu, na kuwaweka wasio haki katika hali ya adhabu hata siku ya hukumu.”
Maandiko yanasema wazi, Bwana huwaokoa watauwa
(watakatifu) na majaribu. Unapopita katika jaribu, kitu cha muhimu kukitunza ni
utakatifu na uhusiano wako na Mungu.
Ayubu mtumishi wa Mungu aliongea kauli ngumu sana.
“mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi, mimi nitarudi tena huko uchi
vile vile; Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana na libarikiwe”.
Ukiichunguza kwa undani kauli hii, utaona kuwa Ayubu hakuvitegemea vitu au mali
zinazoonekana kwa macho bali alivitazamia visivyoonekana kwa macho (2 Wakorintho
4:16-18)
Na zaidi Ayubu alitaka kuulinda na kuutunza
utakatifu wake na uhusiano wake na Mungu. Na ndivyo inavyokupasa mkristo,
usiangalie ni vitu vingapi unavipoteza unapopitia jaribu ulilonalo, bali zidi
kuimarisha uhusiano wako na Mungu ukiulinda utakatifu wako.
Kwa hiyo unapopita katika jaribu lolote ni lazima
uzingatie mambo makuu matatu tuliyojifunza hapo juu, nayo ni; utii wa sauti ya
Mungu, imani na utakatifu. Katika hayo, hakika Mungu atapigana kwa ajili yako
na kukupa ushindi mkuu.
Nina imani umebarikiwa na kupata kitu kipya katika
somo hili ambalo kupitia Roho wa Mtakatifu, Mungu ametufundisha. Shiriki baraka
hizo kwa kushiriki somo hili katika ukurasa wako katika mtandao wowote wa
kijamii.
KUPATA PDF YA SOMO HILI, BONYEZA HAPA
KUPATA MWONGOZO WA KUFANYIKA MTOTO WA MUNGU
(YEHOVA), BONYEZA HAPA
No comments:
Post a Comment