Salamu!
Krismasi ni nini na inapaswa kusherehekewa kwa namna gani?
Kumekuwa na mafundisho mengi sana kutoka kwa wapinga dini (atheists)
na wenye dini tofauti na Ukristo kuhusu siku ya Krismasi. Mafundisho yao mengi
yamekuwa ni kinyume na sherehe hii. Baadhi wamekuwa wakidai hakuna sehemu
katika Biblia inayoturuhusu Wakristo kusherehekea Krismasi kama tunavyofanya.
Na baadhi ya mafundisho yamediriki hata kusema hakuna mitume (watangulizi wetu
wa Kanisa) waliowai kusherehekea sherehe hii.
Maswali tunayopaswa kujiuliza kabla hatujakubali kuyumbishwa
na mafundisho haya ni:-
Kwanini malaika walikwenda kuwapasha habari za kuzaliwa
kwake Yesu Kristo wachungaji usiku ule alipozaliwa?
Kwanini malaika alipowapasha habari wachungaji aliwaambia “I
bring you good news of great joy” akimaanisha “habari njema zenye furaha kuu”?
Kwanini mamajusi na wachungaji walibeba zawadi (manemane,
uvumba na mar’hamu) kumpelekea mototo Yesu?
Maswali hayo yanapatikana katika vitabu vitakatifu vya
Biblia, Mathayo sura ya kwanza na ya pili pamoja na Luka sura ya kwanza.
Inawezekana ndiyo Biblia haisemi chochote kuhusu sherehe za
Krismasi lakini pia haijatukataza kusherehekea Krismasi. Na ikiwa
walioshuhudiwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo (mamajusi na wachungaji) walijawa na
furaha na hata wakampelekea zawadi kwa nini sisi tusifanye sasa? Kwanini
malaika alifanya kazi ya kuwapasha habari wachungaji kama kuzaliwa kwa Yesu
Kristo halikuwa jambo linalostahili kusherehekewa?
Tarehe na majira sahihi ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo bado ni
kitendawili katika maandiko mengi ya Kikristo na hata dini nyingine
zinazomtambua Yesu Kristo. Tarehe 25 ya kila mwezi wa 12 wa mwaka ilibuniwa tu
kwa sababu ya ufanano wa majira ya kuzaliwa halisi kwa Yesu Kristo na majira ya
sehemu mbali mbali duniani. Kwa mujibu wa Teolojia, wakati wa kuzaliwa Yesu
Kristo yalikuwa ni majira ya baridi na kuanguka kwa barafu katika nchi za ulaya
na ndiyo sababu mwezi wa 12 kwa kila mwaka ukachaguliwa kuwa mwezi maalumu wa
sherehe za Krismasi.
Lakini ni namna gani tunapaswa kuisherehekea Krismasi? Krismasi
siyo sherehe ya “birthday” kama inavyodhaniwa na watu wengi na hipaswi
kusherehekewa kama sherehe za “birthday” zetu tunazozisherehekea mara moja kila
mwaka.
Krismasi ni sherehe ya kukubali kulipokea pendo la ukombozi
wa mwanadamu anayepotea katika dhambi kupitia Yesu Kristo ambaye ni Bwana na
Mwokozi wetu. Mwanzo wa pendo hili ni kuzaliwa kwa Mwokozi huyu, Yesu Kristo,
na mwisho wa kukamilika kwa pendo hilo ni katika safari ya msalaba. Kupitia kifo
cha msalaba, dhambi zetu zinatakaswa kwa damu yenye mamlaka ya Yesu Kristo. Na
katika ufufuo wa Yesu Kristo tunakamilishwa na kufanywa wana wa Mungu
tunaoubeba ushindi wa baba yetu manegani mwetu. Ushindi dhidi ya mateso, dhiki,
mauti, magonjwa na shida zote katika dunia hii huku tukiwa na tumaini la wokovu
na uzima wa milele pamoja na Bwana wetu.
Hivyo basi, tunapaswa kuiona siku ya Krismasi kama pendo la
Mungu kwetu wanadamu na hivyo kuisherehekea kwa nguvu zote kwa sababu
tumekubali kulipokea pendo hilo na kufanyika wana wa Mungu. Mungu ameachilia
pendo lake kwa wanadamu wote lakini siyo wote waliokubali kupendwa na
wakapenda. Sisi tuliokubali kupendwa na tumependa hatuna budi kuisherehekea
siku hii ya Krismasi.
Tunawatakia Krismasi njema, pendo la Mungu la zidumu ndani
yetu zaidi tukifanyika baraka kwa wanadamu wenzetu ili wamuone Mungu kupitia
maisha yetu. Amina.
No comments:
Post a Comment