Ni jambo la kawaida kwa wa-Kristo
wengi kuchukulia mambo katika hali ya kawaida pasipo kuchunguza uwepo na/au
makusudi ya jambo au mambo hayo. Mfano mzuri na ndiyo ukweli halisi ni matumizi
ya neno ‘X-mas’, ‘X-MAS’ au ‘Xmas’. Hilo ni neno moja isipokuwa ni tofauti ya
matumizi ya herufi; herufi kubwa au herufi ndogo, lakini neno hilo linatumika
kuwakirisha neno ‘Christmas’.
Mimi pia nilikuwa ni mmoja wa
watumiaji wa neno hilo la kifupi (Xmas) kuwakilisha neno Christmas, inawezekana
unalitumia neno hilo pasipo kujua unamaanisha nini au unalitumia kwa sababu
unafikiri unaokoa wakati kwa kuiandika Christmas kwa neno fupi. Asante kwa dada
yangu aliyenifumbua macho na kunifanya nilifuatilie neno hilo haraka sana.
Ukweli ni kwamba, X inawakilisha
thamani, namba au kitu kisichojulikana katika hisabati (mathematics), na
ukiliangalia neno Christ-mas na X-mas utapata kutambua kuwa herufi X
inawakilisha neno Christ. Na kama X ni thamani, namba au kitu kisichojulikana
katika hisabati (mathematics) na kwetu wa-Kristo, je ni halali kuitumia herufi
isiyojulikana thamani yake kumuwakilisha Kristo? Kwamba hatumjui au hatuijui
thamani ya Kristo?
Funguka macho, acha uvivu, hakikisha
unaandika neno kamili, “Christmas”, tena linaandikwa kwa kuanza na herufi kubwa
‘C’.
Na jambo la pili nililojifunza ni
kumtumia “Santa Claus” katika kipindi hiki cha kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu
Kristo badala ya kumuadhimisha Yesu Kristo mwenyewe. Labda ni kwa sababu
tunahamasisha kupeana zawadi, lakini ukweli ni kwamba tunapaswa tumtamke Yesu
Kristo ambaye ni zawadi tosha maishani mwetu.
Na jambo la mwisho kwa leo ni jinsi
wa-Kristo wengi tunavyosherehekea msimu huu wa sikukuu ya “Christmas” na mwaka
mpya. Tunasherehekea tofauti na inavyotupasa tuisherehekee, tunasherehekea kwa
matendo ya anasa na kujisahau, tumekuwa sawa na watoto wanaofurahi kufika kwa
kipindi hiki kwa sababu watanunuliwa nguo mpya na kula chakula kizuri.
Katika kipindi hiki tunapaswa kufanya
tafakari ya mwaka mzima katika mambo makuu manne; imani, uchumi, jamii,
kurekebisha.
Imani: je, wewe mKristo umeitunza na
kuitetea imani yako pasipo kumtenda Mungu dhambi kwa kipindi chote cha mwaka
unaoumaliza?
Uchumi: je, umepiga hatua kiuchumi
kama ulivyopanga na/au kutegemea wakati unaanza mwaka unaoumaliza?
Jamii: je, uhusiano wako na jamii
unayoishi nayo unakuwa mzuri au unaharibika? Kama una familia, je familia yako
inapata mahitaji muhimu na yale ya ziada kutoka kwako?
Rekebisha: hiki ni kipindi cha
kutambua makosa, mapungufu na kufanya tathmini kwa ujumla. Jitahidi kutambua ni
wapi ulipokwama na tafuta ufumbuzi ili usonge mbele na inapohitajika ushari,
tafuta ushauri kwa watu wanaoweza kukusaidia, usimwambie kila mtu mapungufu
yako. Zaidi mtegemee Mungu.
Mwisho kabisa, ni lazima umshukuru
Mungu; wewe umefika mwishoni mwa mwaka lakini yupo aliyepoteza uhai mwanzoni
mwa mwaka, wewe umejenga nyumba japo ndogo lakini yupo ambaye analala
kibarazani mwa duka la mtu, wewe ulilala njaa usiku mmoja lakini yupo aliyelala
na kushinda njaa kwa zaidi ya siku tatu, wewe unaishi katika nchi yenye amani
lakini yupo anayeishi katikati ya vita, wewe upo huru japokuwa huna kitu lakini
yupo asiye na kitu kama wewe amesingiziwa kesi na kufungwa jela. Huna sababu ya
kukwepa kumshukuru Mungu.
"NAWATAKIENI KHERI YA 'CHRISTMAS' NA FURAHA YA MWAKA MPYA, 2013"