Kila jambo
analokutana nalo mwanadamu lina sababu ya kuwepo, na kuna nguvu inayolishikilia
hilo jambo liendelee kuwepo. Endapo hiyo nguvu itakatwa, basi hilo jambo
haliwezi kuendelea kuwepo. Na uwepo wa nguvu unaosababisha mambo kutendeka
unategemea kanuni; ili usipate magonjwa ya kuambukiza, zipo kanuni za
kujiepusha na magonjwa hayo.
Na katika
mambo ya rohoni, kuna kanuni za kuyapata hayo mambo ya rohoni; ili ubarikiwe,
ule matunda ya kazi za mikono yako na upokee uponyaji ni lazima uzingatie
kanuni. Na kanuni hizo ni; uwe mnyenyekevu kwa Mungu, na unyenyekevu huo
uambatane na maombi, maombi yaliyokusudia kuutafuta na kuuona uso wa Mungu, na
ili uweze kuuona uso wa Mungu ni lazima uachane na njia zote mbaya.
2 Nyakati
17:13-14 “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au
nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu,
watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya;
basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao”.
Hapa neno mvua linabeba
maana mbili;
mvua kwa maana ya mvua, na mvua kama baraka. Na katika baadhi ya vitabu
vitakatifu vya Biblia, Mungu analithibitisha hilo; (Isaya 30:23 Naye atatoa
mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi,
nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ombe zako watakula katika
malisho mapana), mvua kama baraka- Malaki 3:10 “. . . mjue kama sitawafungulia
madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha,
au la”.
Kwa hiyo,
mbingu zikifungwa kusiwe na mvua; mvua kama mvua inaweza isinyeshe na mvua kama
baraka inaweza pia isipatikane. Na ukikosa baraka, basi una laana; inaweza
ikawa ni laana ya ukoo, laana ya kutamkiwa (Mithali 11:26, 24:24,) au ya
kujitamkia kwa kujua au pasipo kujua, au laana inayotokana na kutenda dhambi
(Kumbukumbu la torati 28:15, Malaki 2:2, Zaburi 119:21).
Nzige kula nchi; nzige hula mimea au mazao
yaliyootayo juu ya nchi, wanapokula mazao hula chakula cha binadamu (Zaburi
105:34-35 “Alisema, kukaja nzige na tunutu wasiohesabika wakaila miche yote ya
nchi yao, wakayala matunda ya ardhi yao”).
Unaweza kuwa
na huduma iliyodumaa au imekufa kabisa, unafanya kazi lakini huli matunda
stahili ya kazi yako au wewe ni mkulima lakini mavuno ni hafifu. Katika hali
hizo, nzige wamekula nchi, ni lazima ufanye jambo kuikomboa nchi hiyo; kuinua
au kufufua huduma yako, kunufaika na kazi ya mikono yako na hata kupata mavuno
bora ya mashamba yako. Jambo hili linaweza kusababishwa na nguvu za ufalme wa giza au maisha ya dhambi (Zaburi
119:21), lakini unaweza kujikomboa katika utumwa huo, zingatia kanuni.
Tauni; neno hili linawakilisha magonjwa,
ambayo yanaweza hata kuondoa uhai au kukuacha na ulemavu. Magonjwa yasiyo na
tiba au magonjwa yasiyoeleweka yanasababishwa na nini, na inaweza ikawa ni
malipo ya dhambi (Ayubu 8:3-4, 2 Samweli 24:15) au ni kuonewa na shetani.
Lakini hayo yote yanaweza kukuachilia huru tangu sasa, ikiwa yamekupata wewe au
ndugu yako, Mungu ni mwaminifu hakuwahi kusema uongo hata leo asema uongo.
Katika mambo
hayo matatu; kukosa mvua, nzige kula nchi na tauni, inawezekana ukawa umepitia
jambo moja wapo au yote kwa jinsi tulivyoyaona maana zake katika mwaka huu
(2012) unaomalizika hivi karibuni. Na hungependa kuingia na kutembea na mwaka
unaofuata (2013) na mambo hayo, unatamani kufunguliwa na kuwekwa huru; upokee
baraka kutoka kwa Mungu, kuinua na kufufua huduma yako, kula matunda ya kazi za
mikono yako na kuishi maisha yasiyojua ugonjwa/magonjwa, INAWEZEKANA! Zipo
kanuni alizoziweka Mungu mwenyewe ili tupone, zingatia kanuni hizo. Kanuni hizo
ni:-
Kunyenyekea; ni kutii na kukubali sauti ya Mungu
na kufanya yanayoelekezwa na sauti hiyo (Isaya 1:19 “. . . mkikubali na kutii,
mtakula mema ya nchi”). Sauti ya Mungu siku zote inatuelekeza kuifuata njia
njema, na kuifuata njia njema ni kuchagua mema; baraka, uponyaji, ushindi,
heshima, kuinuliwa na mengine mengi mazuri. Kunyenyekea kunamfanya Mungu atumie
muda wa ziada kututegea sikio na kuyasikiliza maombi yetu, na Mungu
akiyasikiliza maombi yetu lazima tuwe na uhakika wa kupokea majibu (Danieli
12:10, Isaya 66:2).
Kutonyenyekea
kunainua hasira ya Mungu juu ya wanadamu, na ndipo tunapatwa na mabaya (Yeremia
44:10). Kwa hiyo hii ni kanuni ya kwanza, ukitaka kuwa rafiki wa Mungu na
kupokea mema kutoka kwake, lazima unyenyekee.
Kuomba; ni njia ya mwanadamu kuzungumza na
Mungu (Isaya 1:18 “. . . haya njooni tusemezane. . .”), Mungu anaposema ‘njooni
tusemezane’ anatufundisha kuomba ili tupeleke mahitaji yetu kwake na yeye
atujibu kulingana natulivyoomba au tunavyostahili (Yakobo 5:13).
Kuomba ni
kanuni ya pili, ambayo ni lazima iambatane na kanuni ya kwanza (unyenyekevu),
huwezi kuwa muombaji kama hunyenyekei. Unyenyekevu unakupa haki mbele za Mungu,
na maombi ya mwenye haki ndiyo yanayofaa sana (Yakobo 5:16 kuomba kwake mwenye
haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii). Na hii ni kanuni ya pili.
Kuutafuta uso wa Mungu; kama tulivyoona, hizi kanuni zina
mfuatano wa kutegemeana, unapokuwa mnyenyekevu na muombaji ni rahisi sana
kukutana na Mungu. Unapoomba hakikisha umekutana (umekuwa-connected) na Mungu
na ndipo ueleze mahitaji yako. Jambo hili si jepesi, unahitaji kujitoa na
kudhamiria; kuwa mnyenyekevu na muombaji na ndipo utakapokutana na Mungu (Mithali
8:17 . . . na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. Yeremia 29:13 . . .nanyi
mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote). Kanuni ya tatu.
Kuacha njia mbaya; ni kurudi kutoka dhambini na
kumrejea Mungu. Unyenyekevu, maombi na kuutafuta uso wa Mungu ni lazima
viambatane na toba, kila unaposogea mbele za Mungu hakikisha unajitakasa hata
kama hukumbuki kumtenda Mungu dhambi (Hosea 5:15 . . . hata watakapoungama
makosa yao na kunitafuta uso wangu. . .). Ukiamua kuacha njia mbaya, usijiweke
tena katika mazingira ya kuirudia hiyo njia mbaya; epukana na mazingira ya
kutenda dhambi kwa kuangalia, kusikiliza au kuongea (Yeremia 36:7 na kurudi,
kila mtu akiiacha njia yake mbaya. Yeremia 35:15 rudini sasa, kila mtu na
aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu). Na siyo utende dhambi
makusudi kwa kuwa utaomba toba!! Kanuni ya nne.
Ni wewe
mwenyewe, unayeweza kuamua na kujitoa kutoka katika maisha ya mateso na kuonewa
na yule mwovu. Zingatia kufuata, kutenda na kuzitimiza kanuni, amua leo kuingia
mwaka mpya na maisha mapya. Mungu akubariki sana, kwa jina la Yesu Kristo.
Unahitaji kuokoka?
Bonyeza hapa.
Ubarikiwe sanaa Mtumishi wa Mungu kwa somo nzuri nimepata sehemu yangu
ReplyDelete