Wednesday, December 24, 2014

HERI YA KRISMASI NA FURAHA YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO, 2015

 Uongozi wa blogu ya "SILAGO2.BLOG", wachungaji walezi na wapendwa katika pendo liokoalo la Yesu Kristo, tunawatakia wasomaji wetu wote mahali popote mlipo "HERI YA KRISMASI NA FURAHA YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO, 2015".

Kwanza kabisa tunazo shukurani za dhati kwa Mungu aliye hai, aishiye milele, Yehova kupitia Jina la Yesu Kristo kwa kuwa nasi tangu kuanza mwaka wa 2014. Kwa uaminifu, neema na rehema zake ametuvusha salama na kwa imani tutauona mwaka wa 2015. Inawezekana umepoteza wapendwa wako, lakini huna budi kumshukuru na kumtukuza Mungu kwa neema na fadhili zake nyingi alizokutendea.

Pili, tunawashukuru wasomaji na wapenzi wetu wote kwa sababu uwepo wenu ndiyo uwepo wa blogu hii. Mungu wa mbinguni, Yehova awabariki wote na kuwajalizia haja za mioyo yenu kupitia Jina lipitalo majina yote la Yesu Kristo, Amina.

Tatu, tungependa kuwakumbusha kuwa siku kuu za Krismasi na Mwaka mpya zina maana tofauti na jinsi tunavyo zisherehekea. Krismasi ni siku ya kuzaliwa kwa Mfalme, mkombozi wa wanadamu kutoka utumwa wa shetani. hivyo basi, itumie siku hii kuutafakari upendo mkuu wa Mungu na Yesu Kristo kwako, na ukubali kujiachilia moyo wako wazi mbele za Mungu ili "Utatu mtakatifu wa Mungu" uingie na kuishi nawe.
Mwaka mpya ni siku kuu inayotukumbusha neema na rehema za Mungu kwetu, kwamba katika mwaka unaoisha kuna makosa tulimkosea Mungu, lakini bado kwa upendo wake ametuzawadia uzima na afya ambavyo hatukuvistahili kwa kuenenda kwetu katika kutimiza tamaa za miili yetu. Hivyo basi, hatuna budi kutubu, kutengeneza tena uhusiano mzuri na Mungu wetu kupitia damu iokoayo ya Yesu Kristo.

Katika kipindi hiki kifupi cha siku kuu za Krismasi na Mwaka mpya weka historia nzuri ya ushindi, tumia kipindi hiki kujenga umoja, ukaribu na mshikamano, mkiongeza chachu ya upendo na furaha katika familia. Kwa sababu familia yenye amani, furaha na upendo ndiyo familia yenye mafanikio ya kiroho na kimwili.

"KHERI YA KRISMASI NA FURAHA YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO, 2015"


No comments:

Post a Comment

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts