Sunday, September 11, 2016

MWANZO MPYA WA MILELE NDANI YA YESU KRISTO

Ufunuo wa Yohana 21:5
...tazama, nayafanya yote kuwa mapya...

Bwana Yesu asifiwe!
Ninakusalimu kupitia Jina la Yesu Kristo mpendwa msomaji wangu.

Kuna swali napenda ujiulize mpendwa msomaji wangu, leo nakwenda kuongea na mtu mmoja au nafsi moja, naongea na wewe!
SWALI; Licha ya neema, baraka, ulinzi na mema yote Mungu anayokutendea katika maisha yako (Yeremia 29:11-12), kwanini unatenda au unadhamiria kutenda dhambi???
Inawezekana wewe siyo mtu sahihi kwa swali hili, lakini yupo mtu sahihi ambaye ujumbe huu utakwenda kumponya na kumfanya kiumbe kipya. Kama wewe ni mtu sahihi kwa swali hili, je umewahi kujiuliza swali hilo hapo juu??? Viongozi wa dini na hata waumini wenzako wanadhani unaendelea vema, kumbe uliisha jitenga na imani kitambo sana, na yupo mpendwa mwingine anajulika kuwa anatenda dhambi na wapendwa wakimkanya anajifanya kuomba ushahidi, nikuulize swali, umewahi kwenda mbele za Mungu na kumwambia akupe ushahidi wa uovu wako? Najua huwezi kufanya hivyo kwa sababu Mungu hadhihakiwi na hadanganywi na jambo!

Kwa maana hiyo, hauwadanganyi viongozi wako wa dini na wapendwa, haujifichi mbele zao, hauwezi pia kumdanganya au kujificha mbele za Mungu, BALI unaidanganya nafsi yako. Kwanini kujidanganya nafsi basi???

JIBU; ...mungu wa dunia hii (ibilisi/shetani) amepofusha fikira zao, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo...(2 Kor 4:4)
Hakuna mwanadamu atendaye dhambi kwa matakwa yake binafsi, isipokuwa ametiwa upofu nafsini na ndani ya nia yake na ibilisi asione aibu ya dhambi. Kutenda dhambi ni aibu, tena nasema ni aibu, kama ilivyo kwa timamu kutembea bila nguo. Na hii ndiyo sababu dhambi hutendwa kwa kificho, gizani kwani anayepofusha na kumfanya mwanadamu atende dhambi ni mfalme wa giza, shetani au ibilisi. Na mtenda dhambi hutenda dhambi kwa kutimiza matakwa ya ibilisi/shetani...yaani, shetani hutumia mwili wa mwanadamu kutenda dhambi au kufanya uovu; kufanya uzinzi, uasherati, uuaji, wizi, tamaa mbaya iletayo mauti n.k (Waefeso 2:1-2)

Mpenzi msomaji wangu, sihukumu nafsi ya mtu kwa maana sipo katika nafasi ya kuhukumu, mwenye kuhukumu na kurehemu/kusamehe dhambi ni Mungu peke yake kupitia Kristo Yesu. Leo Mungu amekuona, kupitia damu ya Yesu Kristo atakwenda kukusamehe na kukutakasa kabisa.


Dhambi huamsha hasira ya Mungu kwake yeye atendaye dhambi (Waamuzi 2:12,15). Mungu humgeuzia kisogo mtenda dhambi asimtazame...kugeuziwa kisogo na Mungu ni kuondolewa baraka, neema, ulinzi na mema yote ya Mungu maishani mwako kwa maana Malaika watuhudumiao hayo hawawezi kuhudumu kwa mtenda dhambi. Mtu huyu anaachwa peke yake akienenda katika giza na ibilisi, na hufikia wakati wa dhambi sugu iletayo mauti, kwa maana neno linasema, "dhambi ikiisha kukomaa...huzaa mauti" na hapa ndipo aibu huondoka kabisa machoni pa atendaye dhambi. Siyo matakwa ya mwili, bali ni shurutisho la mungu wa dunia hii, ibilisi. Wewe uliyesimama imara, usiwachukie watu wa namna hii, bali waombee. Na wewe utendaye dhambi, kubali kukemewa kwa Jina la Yesu Kristo, Amina.

Mungu ni mwingi wa rehema (Waefeso 2:4), huwarudi wale awapendao kwa namna mbali mbali; 1. kuwatenda mabaya (Waamuzi 2:15), wakati tunapopita katika mateso, majaribu, shida na taabu huwa tunamkumbuka Mungu, na ni kipindi ambacho tunaomba kwa dhati na kumaanisha tukiomba toba kwa uchungu na machozi. Mungu huamua kutupitisha katika nyakati hizo ili kutuweka sawa. 2. Kulituma neno lake liikemee dhambi ndani ya kanisa au kwa mtu binafsi. Hili ni neno la Mungu kwako, fanya hima kuomba toba na kuacha dhambi, Mungu amekuona na anakupenda ndiyo sababu anasema na wewe leo.

Mungu husamehe wale wamuombao toba, haesabu maovu yetu kwa maana anasema, "heri mwisho mzuri kuliko mwanzo mzuri", unapaswa kumaliza kwa ushindi na kuilinda imani (2 Timotheo 4:7). Mungu akiisha kukusamehe huachilia baraka, neema, ulinzi na kila namna ya mema yatokayo kwake katika maisha yako ya kiroho na kimwili (2 Nyakati 7:14)

Mungu anakwenda kufanya mwanzo mpya nawe siku ya leo, anasubiri ukiri kwa kinywa chako ukiwa na imani ndani ya moyo wako na nia ya dhati ukiomba mshamaha/toba na kuachana na dhambi na kuanza mwanzo mpya wa maisha ya imani. Hata kama ulianguka, unayo nafasi pia Mungu siyo mwanadamu, Mungu huuona moyo uliopondeka, moyo uombao toba na kuusamehe pasipo kuhesabu makosa. Neema na rehema za Mungu zatosha kukusamehe na kukutakasa tena, Mungu anasema, "tazama nayafanya yote kuwa mapya...ya kale yamepita" (Ufunuo wa Yohana 21:5)
Mahali pengine anasema, "usiyakumbuke mambo ya kale, tazama nafanya jambo jipya sasa" (Isaya 43:18-19), usibaki katika dhambi na mateso yake, shetani atakuletea mawazo ya kwamba wewe ulitenda dhambi nyingi mno au kubwa sana Mungu hawezi kukusamehe, nakwambia Mungu husamehe dhambi zote, nyingi au chache, kubwa au ndogo. Furahia moyoni mwako kwa maana unakwenda kuanza mwanzo mpya wa imani ndani ya Yesu Kristo.

MAOMBI; (Fuatisha kwa imani maombi haya)
"Yehova, Mungu wa Ibrahimu, Isaka na Yakobo uishie milele, mwingi wa rehema nipo mbele zako sasa mimi mwenye dhambi. Ninakuomba unisamehe na unitakase kwa damu ya Yesu Kristo, damu inenayo mema, ikanene mema katika maisha yangu ya kiroho na kimwili. Ulifute jina langu katika hukumu ya moto na uliandikie katika uzima wa milele. Uiandike upya historia ya maisha yangu, nikaishi maisha matakatifu nikupendeze wewe Mungu wangu, Amina"

Umefanyika kiumbe kipya sasa, ili kuendelea kuukulia wokovu unapaswa utafute kusanyiko la wapendwa linalomuabudu Mungu katika roho na kweli kupitia mwokozi wetu Yesu Kristo, na ujihudhulishe mahali hapo popote pale ulipo mpendwa msomaji wangu.

...uwasamehe na kuwarejeza tena...
2 Nyakati 6:25

No comments:

Post a Comment

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts