Thursday, February 14, 2013

TOBA YA KWELI.



   Kuna tofauti kubwa kati ya toba na toba ya kweli, toba haimalizi kosa/dhambi lakini toba ya kweli inamaliza kosa/dhambi. Na baada ya toba ya kweli, Mungu huzifuta dhambi zetu zote (Isaya 43:25). Unapoamua kufanya toba, fanya toba ya kweli maana hiyo ndiyo toba yenye msamaha wa dhambi ndani yake.

   Toba na toba ya kweli zina sifa kadhaa zinazofanana; kutambua kosa/dhambi, kulijutia na kuliombea msamaha.
Tofauti ya toba na toba ya kweli ni kuacha kuitenda tena dhambi uliyokwisha kuiombea msamaha, hii ndiyo toba anayoipenda na kuitaka Mungu.

TOBA.
   Mathayo 27:3, 5 “Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona amekwisha kuhukumiwa, alijuta akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga”. 

Toba ni kulitambua kosa, kulijutia na kuliombea msamaha. Muomba toba anaweza akayarudia makosa au anaweza akalitambua kosa na akalijutia lakini asiliombee msamaha. Na jinsi unavyorudia kosa au unafanya kosa, unalijutia lakini hauliombei msamaha ndivyo hofu ya Mungu inavyozidi kuondoka ndani yako na dhamira ya kukufanya uitambue dhambi na kuijutia nayo inatoweka. Mtu wa namna hii anafikia mahali anakufa kiroho, na mfu wa roho ni kazi sana kumrudia Mungu. Mtu huyu anahitaji huduma ya ukombozi yenye neema ya Mungu mwenyewe. (Luka 11:24-26).

Shetani ndiye anayewadanganya watu kwamba wametenda dhambi kubwa sana zisizo na msamaha, na hata kuiua dhamira iliyo ndani ya mtu ili mtu huyo asitafute toba ya kweli. 

TOBA YA KWELI.
   Luka 15:11-19 “. . . nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa naye amefufuka, alikuwa amepotea naye ameonekana.”

Toba ya kweli ni kulitambua kosa, kulijutia, kuliombea msamaha na kutolitenda tena. Toba ya kweli urudisha utukufu na hofu ya Mungu kwako. Ili usirudie tena dhambi uliyokwisha iombea msamaha unapaswa kujikita katika maombi na kuepukana na mazingira yasababishayo dhambi hiyo. (Zaburi 1:1-2 na Waefeso 4:28).

Hakuna dhambi isiyo na msamaha kwa Mungu, dhambi zote zinasamehewa kwa sababu neema na rehema za Mungu ni juu ya wanadamu wote, wote tunaweza kusamehewa ikiwa tutafanya toba ya kweli. (Zaburi 103:11-13 na 2 Wakorintho 5:17).

Unataka kumpokea Yesu Kristo leo? Bonyeza hapa.

Monday, December 24, 2012

X-MAS SIYO CHRISTMAS.

Ni jambo la kawaida kwa wa-Kristo wengi kuchukulia mambo katika hali ya kawaida pasipo kuchunguza uwepo na/au makusudi ya jambo au mambo hayo. Mfano mzuri na ndiyo ukweli halisi ni matumizi ya neno ‘X-mas’, ‘X-MAS’ au ‘Xmas’. Hilo ni neno moja isipokuwa ni tofauti ya matumizi ya herufi; herufi kubwa au herufi ndogo, lakini neno hilo linatumika kuwakirisha neno ‘Christmas’.

Mimi pia nilikuwa ni mmoja wa watumiaji wa neno hilo la kifupi (Xmas) kuwakilisha neno Christmas, inawezekana unalitumia neno hilo pasipo kujua unamaanisha nini au unalitumia kwa sababu unafikiri unaokoa wakati kwa kuiandika Christmas kwa neno fupi. Asante kwa dada yangu aliyenifumbua macho na kunifanya nilifuatilie neno hilo haraka sana.

Ukweli ni kwamba, X inawakilisha thamani, namba au kitu kisichojulikana katika hisabati (mathematics), na ukiliangalia neno Christ-mas na X-mas utapata kutambua kuwa herufi X inawakilisha neno Christ. Na kama X ni thamani, namba au kitu kisichojulikana katika hisabati (mathematics) na kwetu wa-Kristo, je ni halali kuitumia herufi isiyojulikana thamani yake kumuwakilisha Kristo? Kwamba hatumjui au hatuijui thamani ya Kristo?

Funguka macho, acha uvivu, hakikisha unaandika neno kamili, “Christmas”, tena linaandikwa kwa kuanza na herufi kubwa ‘C’.

Na jambo la pili nililojifunza ni kumtumia “Santa Claus” katika kipindi hiki cha kumbukumbu ya kuzaliwa Yesu Kristo badala ya kumuadhimisha Yesu Kristo mwenyewe. Labda ni kwa sababu tunahamasisha kupeana zawadi, lakini ukweli ni kwamba tunapaswa tumtamke Yesu Kristo ambaye ni zawadi tosha maishani mwetu.

Na jambo la mwisho kwa leo ni jinsi wa-Kristo wengi tunavyosherehekea msimu huu wa sikukuu ya “Christmas” na mwaka mpya. Tunasherehekea tofauti na inavyotupasa tuisherehekee, tunasherehekea kwa matendo ya anasa na kujisahau, tumekuwa sawa na watoto wanaofurahi kufika kwa kipindi hiki kwa sababu watanunuliwa nguo mpya na kula chakula kizuri. 

Katika kipindi hiki tunapaswa kufanya tafakari ya mwaka mzima katika mambo makuu manne; imani, uchumi, jamii, kurekebisha. 

Imani: je, wewe mKristo umeitunza na kuitetea imani yako pasipo kumtenda Mungu dhambi kwa kipindi chote cha mwaka unaoumaliza?

Uchumi: je, umepiga hatua kiuchumi kama ulivyopanga na/au kutegemea wakati unaanza mwaka unaoumaliza?

Jamii: je, uhusiano wako na jamii unayoishi nayo unakuwa mzuri au unaharibika? Kama una familia, je familia yako inapata mahitaji muhimu na yale ya ziada kutoka kwako?

Rekebisha: hiki ni kipindi cha kutambua makosa, mapungufu na kufanya tathmini kwa ujumla. Jitahidi kutambua ni wapi ulipokwama na tafuta ufumbuzi ili usonge mbele na inapohitajika ushari, tafuta ushauri kwa watu wanaoweza kukusaidia, usimwambie kila mtu mapungufu yako. Zaidi mtegemee Mungu. 

Mwisho kabisa, ni lazima umshukuru Mungu; wewe umefika mwishoni mwa mwaka lakini yupo aliyepoteza uhai mwanzoni mwa mwaka, wewe umejenga nyumba japo ndogo lakini yupo ambaye analala kibarazani mwa duka la mtu, wewe ulilala njaa usiku mmoja lakini yupo aliyelala na kushinda njaa kwa zaidi ya siku tatu, wewe unaishi katika nchi yenye amani lakini yupo anayeishi katikati ya vita, wewe upo huru japokuwa huna kitu lakini yupo asiye na kitu kama wewe amesingiziwa kesi na kufungwa jela. Huna sababu ya kukwepa kumshukuru Mungu.

 "NAWATAKIENI KHERI YA 'CHRISTMAS' NA FURAHA YA MWAKA MPYA, 2013"

Sunday, December 16, 2012

KANUNI ZA KUISHI MAISHA YA USHINDI NA BARAKA.



   Kila jambo analokutana nalo mwanadamu lina sababu ya kuwepo, na kuna nguvu inayolishikilia hilo jambo liendelee kuwepo. Endapo hiyo nguvu itakatwa, basi hilo jambo haliwezi kuendelea kuwepo. Na uwepo wa nguvu unaosababisha mambo kutendeka unategemea kanuni; ili usipate magonjwa ya kuambukiza, zipo kanuni za kujiepusha na magonjwa hayo.

   Na katika mambo ya rohoni, kuna kanuni za kuyapata hayo mambo ya rohoni; ili ubarikiwe, ule matunda ya kazi za mikono yako na upokee uponyaji ni lazima uzingatie kanuni. Na kanuni hizo ni; uwe mnyenyekevu kwa Mungu, na unyenyekevu huo uambatane na maombi, maombi yaliyokusudia kuutafuta na kuuona uso wa Mungu, na ili uweze kuuona uso wa Mungu ni lazima uachane na njia zote mbaya.

2 Nyakati 17:13-14 “Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao”.

   Hapa neno mvua linabeba maana mbili; mvua kwa maana ya mvua, na mvua kama baraka. Na katika baadhi ya vitabu vitakatifu vya Biblia, Mungu analithibitisha hilo; (Isaya 30:23 Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng’ombe zako watakula katika malisho mapana), mvua kama baraka- Malaki 3:10 “. . . mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la”.

Kwa hiyo, mbingu zikifungwa kusiwe na mvua; mvua kama mvua inaweza isinyeshe na mvua kama baraka inaweza pia isipatikane. Na ukikosa baraka, basi una laana; inaweza ikawa ni laana ya ukoo, laana ya kutamkiwa (Mithali 11:26, 24:24,) au ya kujitamkia kwa kujua au pasipo kujua, au laana inayotokana na kutenda dhambi (Kumbukumbu la torati 28:15, Malaki 2:2, Zaburi 119:21).

   Nzige kula nchi; nzige hula mimea au mazao yaliyootayo juu ya nchi, wanapokula mazao hula chakula cha binadamu (Zaburi 105:34-35 “Alisema, kukaja nzige na tunutu wasiohesabika wakaila miche yote ya nchi yao, wakayala matunda ya ardhi yao”). 

Unaweza kuwa na huduma iliyodumaa au imekufa kabisa, unafanya kazi lakini huli matunda stahili ya kazi yako au wewe ni mkulima lakini mavuno ni hafifu. Katika hali hizo, nzige wamekula nchi, ni lazima ufanye jambo kuikomboa nchi hiyo; kuinua au kufufua huduma yako, kunufaika na kazi ya mikono yako na hata kupata mavuno bora ya mashamba yako. Jambo hili linaweza kusababishwa na nguvu  za ufalme wa giza au maisha ya dhambi (Zaburi 119:21), lakini unaweza kujikomboa katika utumwa huo, zingatia kanuni.

   Tauni; neno hili linawakilisha magonjwa, ambayo yanaweza hata kuondoa uhai au kukuacha na ulemavu. Magonjwa yasiyo na tiba au magonjwa yasiyoeleweka yanasababishwa na nini, na inaweza ikawa ni malipo ya dhambi (Ayubu 8:3-4, 2 Samweli 24:15) au ni kuonewa na shetani. Lakini hayo yote yanaweza kukuachilia huru tangu sasa, ikiwa yamekupata wewe au ndugu yako, Mungu ni mwaminifu hakuwahi kusema uongo hata leo asema uongo.

Katika mambo hayo matatu; kukosa mvua, nzige kula nchi na tauni, inawezekana ukawa umepitia jambo moja wapo au yote kwa jinsi tulivyoyaona maana zake katika mwaka huu (2012) unaomalizika hivi karibuni. Na hungependa kuingia na kutembea na mwaka unaofuata (2013) na mambo hayo, unatamani kufunguliwa na kuwekwa huru; upokee baraka kutoka kwa Mungu, kuinua na kufufua huduma yako, kula matunda ya kazi za mikono yako na kuishi maisha yasiyojua ugonjwa/magonjwa, INAWEZEKANA! Zipo kanuni alizoziweka Mungu mwenyewe ili tupone, zingatia kanuni hizo. Kanuni hizo ni:-

   Kunyenyekea; ni kutii na kukubali sauti ya Mungu na kufanya yanayoelekezwa na sauti hiyo (Isaya 1:19 “. . . mkikubali na kutii, mtakula mema ya nchi”). Sauti ya Mungu siku zote inatuelekeza kuifuata njia njema, na kuifuata njia njema ni kuchagua mema; baraka, uponyaji, ushindi, heshima, kuinuliwa na mengine mengi mazuri. Kunyenyekea kunamfanya Mungu atumie muda wa ziada kututegea sikio na kuyasikiliza maombi yetu, na Mungu akiyasikiliza maombi yetu lazima tuwe na uhakika wa kupokea majibu (Danieli 12:10, Isaya 66:2). 

Kutonyenyekea kunainua hasira ya Mungu juu ya wanadamu, na ndipo tunapatwa na mabaya (Yeremia 44:10). Kwa hiyo hii ni kanuni ya kwanza, ukitaka kuwa rafiki wa Mungu na kupokea mema kutoka kwake, lazima unyenyekee.

   Kuomba; ni njia ya mwanadamu kuzungumza na Mungu (Isaya 1:18 “. . . haya njooni tusemezane. . .”), Mungu anaposema ‘njooni tusemezane’ anatufundisha kuomba ili tupeleke mahitaji yetu kwake na yeye atujibu kulingana natulivyoomba au tunavyostahili (Yakobo 5:13). 

Kuomba ni kanuni ya pili, ambayo ni lazima iambatane na kanuni ya kwanza (unyenyekevu), huwezi kuwa muombaji kama hunyenyekei. Unyenyekevu unakupa haki mbele za Mungu, na maombi ya mwenye haki ndiyo yanayofaa sana (Yakobo 5:16 kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii). Na hii ni kanuni ya pili.

   Kuutafuta uso wa Mungu; kama tulivyoona, hizi kanuni zina mfuatano wa kutegemeana, unapokuwa mnyenyekevu na muombaji ni rahisi sana kukutana na Mungu. Unapoomba hakikisha umekutana (umekuwa-connected) na Mungu na ndipo ueleze mahitaji yako. Jambo hili si jepesi, unahitaji kujitoa na kudhamiria; kuwa mnyenyekevu na muombaji na ndipo utakapokutana na Mungu (Mithali 8:17 . . . na wale wanitafutao kwa bidii wataniona. Yeremia 29:13 . . .nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote). Kanuni ya tatu.

Kuacha njia mbaya; ni kurudi kutoka dhambini na kumrejea Mungu. Unyenyekevu, maombi na kuutafuta uso wa Mungu ni lazima viambatane na toba, kila unaposogea mbele za Mungu hakikisha unajitakasa hata kama hukumbuki kumtenda Mungu dhambi (Hosea 5:15 . . . hata watakapoungama makosa yao na kunitafuta uso wangu. . .). Ukiamua kuacha njia mbaya, usijiweke tena katika mazingira ya kuirudia hiyo njia mbaya; epukana na mazingira ya kutenda dhambi kwa kuangalia, kusikiliza au kuongea (Yeremia 36:7 na kurudi, kila mtu akiiacha njia yake mbaya. Yeremia 35:15 rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu). Na siyo utende dhambi makusudi kwa kuwa utaomba toba!! Kanuni ya nne.

Ni wewe mwenyewe, unayeweza kuamua na kujitoa kutoka katika maisha ya mateso na kuonewa na yule mwovu. Zingatia kufuata, kutenda na kuzitimiza kanuni, amua leo kuingia mwaka mpya na maisha mapya. Mungu akubariki sana, kwa jina la Yesu Kristo.

Unahitaji kuokoka? Bonyeza hapa.

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts