Manung’uniko ni dalili ya kukata tamaa na kukiri kukosa
tumani la jambo au hali ngumu anayoipitia mtu. Japokuwa mtu huyo anaweza
asikiri kukata tamaa kwa kinywa chake, lakini kwa kupitia manung’uniko anakiri
kukata tamaa na kukosa msaada japo siyo kwa ukiri wa moja kwa moja.
Katika maisha ya kiroho haipaswi kunung’unikia hali ya
maisha au majaribu unayopitia, hasa haipaswi kumnung’unikia Mungu. Kwa sababu,
kama nilivyokwisha kueleza hapo mwanzo, manung’uniko ni dalili ya kukiri kukata
tamaa na kukosa mwelekeo.
Ni afadhari ujilaumu na kujinung’unikia nafsi yako wewe
mwenyewe na siyo kumnung’unikia Mungu. Mtumishi wa Mungu, Ayubu alipofikwa na
jaribu zito la kupotelewa na watoto, wanyama na kupata ugonjwa mbaya wa ajabu
hakuthubutu kumlaumu au kumnung’unikia Mungu kwa kinywa chake au kwa moyo wake.
Hebu tuangalie maandiko yafuatayo;
Ayubu 1:20. Ndipo Ayubu akainuka akalirarua joho lake, kisha
akanyoa kichwa chake, na kuanguka na
nchi na kusujudia; akasema, Mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi,
name nitarudi tena huko uchi vile vile; Bwana alitoa na Bwana ametwaa; jina la
Bwana na libarikiwe. Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi, wala
hakumwazia Mungu kwa upumbavu.
Ni neno la kuajabisha sana, baada ya Ayubu kupata habari ya
kupotelewa watoto wake wote na mali yake yote, alirarua joho lake, akanyoa
kichwa chake, akaanguka na kusujudu. Kwa
kurarua joho lake na kunyoa kichwa chake alionesha utii na unyenyekevu mbele za
Mungu.
Ayubu alionesha utii kwa Mungu kwa sababu alijua, watoto
wake na mali zake alivipata kwa sababu Mungu alimbariki vitu hivyo. Na ndani ya
moyo wake, Ayubu alimsujudia Mungu kwa sababu huyo ndiye aliyebaki naye, na
Mungu ndiyo tumaini na msaada wake tu.
Ayubu 3:1. Baada ya hayo Ayubu akafunua kinywa chake, na
kuilaani siku yake.
Ilipofikia wakati moya wa Ayubu ulipotaka kunung’unika na
kusononeka, Ayubu aliona ni vema ailaani siku yake ya kuzaliwa lakini
hakuthubutu kumlaani au kumnung’unikia Mungu wa mbinguni aliyemuumba.
Unapomnung’unikia au kumlaani Mungu kwa mambo magumu
unayoyapitia au unayokutana nayo katika maisha yako, unafanya kosa kubwa sana.
Ni busara endapo utamuuliza Mungu nini makusudi ya mapito haya, ili kama ni vita
dhidi ya shetani, Mungu atakuelekeza jinsi ya kuvipigana na kwa Jina la Yesu
Kristo utashinda kwa ushindi mkubwa.
Hebu tuangalie neno la Mungu (kutoka kinywani mwa Bwana)
linasemaje kuhusu manung’uniko;
Hesabu 14:26-38. 26. Kisha Bwana akanena na Haruni na Musa
na kuwaambia, 27. Je nichukuliane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata
lini? Nimesikia manung’uniko ya wana wa Israeli, waninung’unikiayo. 28. Waambieni,
kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni
mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi; 29. Mizoga yenu itaanguka katika jangwa
hili,
30. Hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo
niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa
Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.
34. kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani,
siku arobaini, kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka
arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu.
Katika kifungu hicho cha Biblia hapo juu tunajifunza vitu
vikuu vipatavyo vine, navyo ni kama vifuatavyo;
Manung’uniko ni uovu mbele za Mungu
“Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung’unikiao hata
lini?”, maneno hayo ya Mungu yanapatikana katika Hesabu 14:26. Maneno na mawazo
yanayoambatana na manung’uniko ndiyo hufanyika uovu mbele za Mungu. Watu wengi
wanapo nung’unika hutamka maneno au huwaza mawazo ya kumlaani Mungu, na wakati
mwengine kuwalaani na kuwaumiza wengine. Hapo ndipo manung’uniko yanapokuwa ni
uovu mbele za Mungu.
Na mara nyingi, manung’uniko yanaambatana na kukata tamaa,
na kukata tamaa mar azote huwa ni chanzo cha kutenda dhambi kwa namna moja au
nyingine. Kwa maana hiyo; manung’uniko huzaa kukata tamaa na kukata tamaa huzaa
dhambi, dhambi ni uovu na chukizo mbele za Mungu.
Kwa mfano; mwanadamu anapo kata tamaa kutokana na ugumu wa
maisha, hutafuta njia haramu ya kumuwezesha kuishi kama kufanya ukahaba, wizi
na ujambazi, mauaji n.k. hayo yote huja baada ya mtu huyu kunung’unika kuhusu
ugumu wa maisha, baada ya kukosa majibu hufikia kukata tamaa inayopelekea
kuchukua maamuzi yasiyo sahihi ambayo ni dhambi na chukizo mbele za Mungu kama
tulivyoona katika mfano hapo juu.
Manung’uniko husababisha kifo
“mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili”, Hesabu 14:29. Kuna
aina mbili za vifo; kifo cha kimwili na kifo cha kiroho.
Maisha ya dhambi yanayotokana na kukata tamaa baada ya
manung’uniko ya muda mrefu, hupelekea kifo cha kimwili na kiroho. Kifo cha
kiroho ni kurudi nyuma baada ya kupokea wokovu wa Yesu Kristo, unapoishi maisha
ya dhambi unakuwa umerudi nyuma kiroho au umeanguka dhambini. Na kifo cha
kimwili hufuatia kama matokeo ya maisha ya dhambi unayoyaishi.
Haimaanishi
wasiotenda dhambi hawafi, la hasha, bali maisha ya dhambi humpeleka mtu
kaburini pasi na umri timilifu (Ayubu 5:26, Ayubu 42:16-17). Yohana 8:21(b),
nanyi mtakufa katika dhambi yenu. Kama tulivyoona hapo juu; manung’uniko huzaa
kukata tamaa, kukata tamaa huzaa dhambi na dhambi huzaa kifo, kinachoweza kuwa
cha kiroho au cha kimwili.
Kutofikia au kutotimiza malengo yako au makusudi ya Mungu
katika maisha yako
“hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua
mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo”, Hesabu 14:30.
Hayo yalikuwa ni maneno ya Mungu kwa wana wa Israeli, na
kama tulivyoona hapo juu; manung’uniko husababisha kukata tamaa na kukata tamaa
husababisha kutenda dhambi na dhambi hupelekea mauti ya kiroho au ya kimwili au
vyote kwa pamoja.
Unapokufa kiroho, unauwa makusudi ya Mungu katika maisha
yako. Na Mungu asivyo na hasara wewe mmoja unaporudi nyuma, anainua jeshi kubwa
la watu kumtumikia.
Yesu Kristo alipoambiwa awatulize wanafunzi wake waliokuwa
wakimsifu, na Mafarisayo; alijibu; “Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe
yatapiga kelele”, hapo Yesu alikuwa akitufundisha kuwa, tunapokata tamaa na
kuuwa huduma zetu, Mungu anainua watu wengine ili kuiendeleza kazi yake. Kazi
ya Mungu haifi hata siku moja, ukizira wewe, atafanya mwingine, maadam utukufu
umrudie Mungu.
Aidha unapokuwa na malengo katika maisha yako, kunung’unika
kunakopelekea kukata tamaa inayosababisha dhambi na hatimaye kifo cha kimwili,
kunazima malengo yako na kufuta kabisa ndoto zako maishani. Na kusababisha
kizazi chako kifuatacho kurithi laana zako, isipokuwa kitatubu na kutakaswa
kutoka katika vifungu na maisha ya laana.
Manung’uniko huchelewesha makusudi ya Mungu au mafanikio
yako katika maisha
“kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani,
siku arobaini, kila siku kuhesabiwa mwaka”, Hesabu 14:34
Wana wa Israeli waliipeleleza nchi ya ahadi kwa muda wa siku
arobaini, waliporudisha habari ya nchi hiyo ndipo walipomlalamikia na
kumnung’unikia Mungu na kusema ingekuwa heri kama wangalikufa katika nchi ya
utumwa ya Misri ama wangalikufa jangwani (Hesabu 14:1-3).
Hata wewe mpendwa msomaji wangu, inawezekana uko katika
wakati mgumu, unapitia majaribu mazito unayodhani huwezi kuyavuka. Unafikia
hatua unakata tamaa, unamlaumu Mungu kwa nini alikuumba, ni heri ufe sasa.
Ninakwambia sasa, acha kumlaumu Mungu, acha sasa kumlaani
Mungu, acha kukata tamaa, usithubutu kurudi nyuma, kwa Jina la Yesu Kristo,
yupo Mungu ili akusaidie na utasema hakika wewe Mungu umekuwa ni Ebeneza
kwangu.
Ikiwa Mungu anayo makusudi na maisha yako, mafanikio yako au
baraka zako ni lazima akupitishe katika kipimo cha uvumilivu na uaminifu,
unapofuzu mtihani huo ndipo Mungu anapoachilia kibari katika maisha yako,
huduma yako na baraka zako.
Nataka nikupe angalizo katika somo hili; siyo kila mtihani
au magumu unayopitia ni makusudi ya Mungu. Muulize Mungu nini chanzo, sababu na
makusudi ya hali unayopitia.
Ikiwa ni uonevu wa ibilisi, mwambie Mungu akupiganie na
akupe kuyashinda yote katika Jina la Yesu Krsito.
Ikiwa ni makusudi ya Mungu upitie hatua uliyopo sasa,
imekupasa kuvumilia yote, usilalamike, usinung’unike, usikate tamaa wala
usimlaani Mungu. Simama imara kuitetea imani yako.
Tukichukua mfano wa wana wa Israeli, Mungu aliwapitisha
jangwani katika hali ngumu kwa makusudi maalumu;
Kutoka 7:16. “Nawe umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania,
amenituma nije kwako, kusema, wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia
jangwani”,
Mungu hakuwapitisha wana wa Israeli jangwani kwa bahati
mbaya, aliwapitisha kwa makusudi maalumu. Kumbuka Mungu aliahidi kuwapa nchi
yenye maziwa na asali (nchi ya ahadi), ili kuifikia ile nchi, iliwapasa kupitia
mtihani mzito jangwani.
Kule kuenenda kwao jangwani; kwa kumsifu Mungu aliyewatoa
utumwani na sasa anakwenda kuwapa nchi ya ahadi au kwa kumlalamikia na
kumnung’unukia Mungu, ndiko kuliamua ni nani ataingia na nani hataingia katika
nchi ya ahadi.
Na hii ni kwako pia mpendwa mwenzangu, vile unavyomuona
Mungu katika mtihani unaoupitia ndio kunaamua ni jinsi gani utafikia ahadi ya
ukombozi ya Mungu iliyopo mbele yako. Ikiwa unamlalamikia, unamlaani Mungu au
unakata tamaa, ni dhairi utashindwa kufikia baraka na mafanikio yako ambayo
Mungu ameyaweka mbele zako baada ya kuimaliza safari ya mtihani unaoupitia, ama
utaifikia kwa wakati wa kuchelewa hadi hapo Mungu atakapojiridhisha kuwa
umekomaa.
Hebu tuangalie neno la Mungu kuhusu mitihani tunayoipitia;
“Amri hii ninayokuamuru leo mtaishika kuitenda, mpate kuishi na kuongezeka, na
kuingia katika ile nchi amabayo Bwana aliwaapia baba zenu; nanyi mtaimiliki.
Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako, aliyokuongoza miaka hii
arobaini katika jangwa, ili akutweze, kukujaribu, kuyajua yaliyo moyoni mwako,
kwamba utashika amri zake, au sivyo”, Kumbukumbu la Torati 8:1-2.
Nikupe mfano mfupi; matajiri wengi wanaotumia fedha na mali
zao kuwatunza yatima na maskini, historia ya maisha yao ni watu waliotokea
katika hali ngumu sana za kiuchumi. Mungu anapo wabariki na kuwapa mali,
anawakumbusha kule walikotokea kisha anaweka mzigo wa watu hao kumtumikia Mungu
kwa kutumia fedha na mali zao katika kuwatunza yatima na maskini.
Ili Mungu akubariki baraka za kiroho ni lazima akupitishe
katika mtihani wa kukataliwa, watumishi wakubwa unaowaona leo kuna kipindi
kigumu walichokipitia hata kufikia hapo unapowaona wamefika na unapotamani na
wewe ufikie. Wapo wachungaji walioanza kanisa na watu wa familia zao tu kwa
miaka kadhaa kabla hawajafikia kuwa na wafuasi zaidi ya miatano.
Na wapo wahubiri wakubwa ambao wakihubiri maelfu ya watu
wanaokoka, walianza kwa mikutano ambayo walihubiri na hakuna mtu hata mmoja
aliyeokoka.
Nataka nikwambie, hawakukata tamaa, hawakumlaumu wala
kumnung’unikia Mungu, bali waliendelea kumtukuza, kumuhimidi na kumtumaini
Mungu katika huduma zao.
Vivyo hivyo, ili Mungu akubariki baraka za kimwili kama
fedha na mali, ni lazima akupitishe katika mtihani wa dhiki ya kukosa fedha na
mali. Ili akupie moyo wako una mtazamo gani kumuelekea Mungu. Ikiwa unakata
tamaa, unamnung’unikia Mungu, ujue hutafikia baraka ambazo Mungu ameziweka
mbele yako, na ikiwa kwa neema ya Mungu utazifikia baraka hizo, basi utachelewa
sana.
Katika kumalizia, ninataka nikutie nguvu mpendwa, usikate
tamaa, usimlaumu wala usimnung’unikie Mungu. Simama imara katika mtihani
unaoupitia, yupo Mungu jina lake anaitwa Yehova, atakusaidia na kukutetea ikiwa
tu utamtumainia na kumtegemea yeye. Hakika upo ushindi na baraka baada tu ya
kuumaliza mtihani wako, usithubutu kurudi nyuma kiimani na kumuacha Mungu na
wala usithubutu kukata tamaa ya maisha, shindig upo, katika Jina la Yesu
Kristo. Amina.
Kudownload somo hili katika PDF, bonyeza HAPA
Kudownload somo hili katika PDF, bonyeza HAPA