Friday, November 9, 2012

MSAMAHA.


   Msamaha ni kufuta au kuachilia mzigo wa makosa unayotendewa na mtu pasipo kuhesabu ni mara ngapi mtu huyo amekukosea.
Isaya 43:25 “Mimi, naam, mimi ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe; wala sitazikumbuka dhambi zako”.
Hapo neno la Mungu linatufundisha kuwa; msamaha ni kuyafuta makosa (dhambi) na kutoyakumbuka tena.
Luka 6:37b “…achilieni, nanyi mtaachiliwa”.
Hapa tunaona kuwa maana nyingine ya msamaha ni kuachilia; mtu anaposhindwa kusamehe anabeba mzigo wa hasira ndani ya moyo wake, ambapo mzigo huu unaweza kumfanya mtu huyu akose raha, amani na hata furaha. Hapo Mungu anatuambia tuachilie na kutua mizigo iliyo ndani ya mioyo yetu.
AINA ZA MSAMAHA.
Kuna aina mbili za kusamehe, aina hizi ni;
(a). Msamaha wa kidunia.
Huu ni msamaha wa kusamehe na kutosahau. Msamaha huu hautokani na Mungu, na haukubaliki mbele za Mungu.
Ni msamaha wa kinafiki, mtu anakwambia amekusamehe lakini ndani ya moyo wake ana uchungu nawe. Msamaha huu unahesabu makosa, na wengu wameumia kwa sababu ya kusamehe kwa kutumia msamaha wa aina hii. Unapomwambia mtu nimekusamehe na kumbe bado una uchungu naye, yeye anapata amani na furaha lakini wewe unajawa na uchungu na hasira inayokufanya uumie moyo.
Wengi wetu tumekuwa na msamaha wa aina hii, Mungu atusaidie tuwe na msamaha wa Kimungu kwani msamaha huu una raha na faida. Kuna watu wamekonda na hawana raha siyo kwa sababu ya maisha magumu, bali ni kwa sababu wanavinyongo na mizigo mizito ndani ya mioyo yao.
(b). Msamaha wa Kimungu.
   Huu ni msamaha wa kusamehe na kusahau kabisa. Msamaha huu ni wa Mungu na unatokana na Mungu mwenyewe, kwani Mungu anasema yeye anatusamehe na kusahau kabisa makosa yetu (Isaya 43:25). Nasi kama watoto wa Mungu tunapaswa kuwa na tabia ya Mungu katika kusamehe, tunapaswa tusamehe na kusahau yote tunayokosewa na wenzetu.

Saturday, October 27, 2012

AHADI YA MUNGU HUTUJENGEA IMANI ITUPAYO HAKI.


Ahadi za Mungu.
   Mungu amefanya ahadi nyingi kwa mwanadamu; ahadi za uponyaji, mafanikio, heshima, hekima, ufaulu katika masomo na nyingine nyingi. Na wengi wetu tunazifahamu vizuri ahadi hizo alizotuahidi Mungu; tunazisoma katika neno lake takatifu, Biblia na pia tunazisikia kupitia watumishi mbalimbali wa Mungu.
Zaburi 23:4 “Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya, Kwa maana wewe upo pamoja nami”,  na  Zaburi 119:50 “Hii ndiyo faraja yangu katika taabu yangu, Ya kwamba ahadi yako imeniuhisha”.
   Kupita kati ya bonde la uvuli wa mauti (Zaburi 23:4) na kuwa katika taabu (Zaburi 119:50) ni kuingia au kupitia katika hali zenye changamoto mbalimbali za kiafya; magonjwa na udhaifu wa mwili, kielimu; kushindwa kutimiza malengo yako, kiuchumi; hali ngumu ya kiuchumi au kukosa ajila licha ya kuwa na elimu stahiki, kijamii; kukosa watoto kwa miaka mingi katika ndoa na hata jamii inakuita tasa, kufiwa na watoto pale tu wanapozaliwa na changamoto za namna nyingine nyingi. Katika neno la Mungu hapo juu tunafundishwa kwamba kuna nyakati tutaingia katika changamoto, taabu au bonde la uvuli wa mauti katika maisha yetu. Jambo la kujiuliza hapa, je tuingiapo katika changamoto au taabu hizo tunachukua hatua gani? Je, tumekuwa ni watu wa kumlaumu Mungu kwanini ameruhusu tuingie katika taabu? Na kama tumekuwa ni watu wa kulaumu na tunasubiri majibu kutoka kwa Mungu hakika Mungu hata tujibu kamwe, kwa sababu Mungu hana majibu ya lawama. Mungu anayo majibu ya maneno au maombi yenye hoja zilizojengwa katika imani ya neno lake tu.
   Na ndiyo maana kupitia mistari ya neno la Mungu hapo juu anatufundisha kuwa na imani kwa ahadi zake kwetu.  Anaposema “sitaogopa mabaya, kwa maana wewe upo pamoja nami”, Mungu kuwa pamoja naye ni kwamba ahadi ya Mungu ya ukombozi imemfunika na ni lazima atatoka katika bonde hilo la uvuli wa mauti, na “ahadi yako imeniuhisha” anamaanisha hawezi kukata tama pasipo kujali anapitia taabu ya namna gani kwa sababu ukombozi wake unakuja tena uko karibu.
   Na sisi tunapopitia katika mahangaiko, taabu, shida na misukosuko ya maisha tusiwe ni watu wa kulaumu na kulalamika mbele za Mungu, bali tuwe ni watu wenye kusimama katika maombi yenye imani ya ukombozi tukiziangalia ahadi za Mungu katika taabu zetu.

Thursday, September 27, 2012

NGUVU YA MANENO.


  Katika maneno tunayoyazungumza kuna nguvu ya uumbaji wa kile tunachokizungumza. Kwa mfano mtumishi wa Mungu anapofanya maombezi kwa ajili ya mtu fulani, anatamka maneno ya uponyaji kwa imani, na yule anayeombewa akiyasikia yale maneno ya uponyaji anaamini katika maneno yale na ndipo anapokea uponyaji. Hii inatokea kwa sababu maneno tunayoyasikia yanatufanya tujenge picha ya kile tunachokisikia. Ukisikia maneno ya uponyaji unapata picha ya kupona, ukisikia maneno ya kukutia moyo unapata picha ya kutiwa moyo na ukisikia maneno ya kukukatisha tamaa utapata picha ya kukata tamaa na kushindwa. Na jambo hilo linasababishwa na jinsi tunavyojenga imani katika maneno tunayoyasikia ama kujisemea wenyewe.
Yakobo 1:19 “Basi kila mtu  na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema;”.
Mstari huo wa kitabu kitakatifu cha Biblia, unatufundisha kutokuwa wepesi wa kusema. Kwa sababu katika kusema sana tutasema maneno yenye kuvunja moyo, kukatisha tamaa, kulaani na hata maneno yasiyo na maana ili mradi tuonekane tumesema. Tunatakiwa tuseme au tuongee maneno ya kubariki, kutia moyo na kufariji; maneno ambayo mtu anayekusikia atatamani akusikie tena na kesho na siku inayofuata kwa sababu una kitu cha maana katika maisha yake.
   Baraka, kwa kutumia maneno ya vinywa vyetu tunaweza kubariki. Tukitaka kumbariki mtu au kumfariji tunatumia maneno. Tunatamka maneno yenye baraka au kufariji. Mwanzo 27:27-28 “…akambariki AKASEMA (maneno), Mungu na akupe  ya umande wa mbingu, na ya manono ya nchi, na wingi wa nafaka na mvinyo.”
   Laana, pia kwa kututmia maneno ya vinywa vyetu tunaweza tukatamka maneno ya kulaani. Ambapo tunaweza kujilaani wenyewe au wenzetu kwa kujua ama kutokujua. Tunapoongea jambo baya kwa maisha yetu au ya wenzetu tunakuwa tunatamka laana ambazo ni lazima zitatimia. Zaburi 10:7 “kinywa chake kimejaa laana, na hila na dhuluma, chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu.”
   Ikiwa unatamka laana au baraka, ushindi au kushindwa katika maisha yako au ya mtu mwingine, ni lazima jambo hilo litakuja kutimia. Unaweza ukamwambia mtu fulani kuwa unataka uanze kufanya biashara, na mtu huyo akakwambia, “na wewe unataka kufanya biashara, ameshinwda fulani utaweza wewe?” badala ya kumjibu NITAWEZA, unamjibu ‘najaribu jaribu tu ndugu yangu’. Unaanza biashara alafu miaka inakatika huoni faida yoyote, ni kwa sababu uliyemshirikisha jambo lako aliongea kushindwa na wewe pia ukakiri kushindwa huko. Kwa maana hiyo unaweza ukawa umetamkiwa/umejitamkia laana au baraka katika maisha yako bila wewe kujua. Na falme zote mbili; ufalme wa giza na Ufalme wa Mungu zinafuatilia unayoyakili kwa ajili ya maisha yako au ya wenzako ili kuyatenda au kuhakikisha yanatendeka.
Isaya 59:17(a) “Mimi nayaumba matunda ya midomo;”. Hapa Mungu alimwambia nabii Isaya kuwa yeye (Mungu), anayaumba matunda ya midomo yetu, kwa maana nyingine ni kwamba Mungu anayaumba maneno tunayotamka kwa ajili ya maisha yetu au wenzetu.
Na kwa upande wa ufalme wa giza pia yapo mapepo yanayofuatilia na kutimiza maneno ya vinywa vyetu, hasa maneno ya laana ili kuhakikisha tunaishi maisha yenye mateso na dhiki.
Kwa hiyo ndugu mpendwa katika Kristo Yesu, unatakiwa kufanya maombi ya kufunga ili uvunje laana zote katika maisha yako, laana ulizojitamkia kwa kujua au kutokujua na zile walizokutamkia wengine. Na Mungu yupo atakujibu na kukubariki, muamini tu.

Saturday, September 15, 2012

MAKUSUDI YA KUUMBWA MWANADAMU


   Baada ya Lucifer (ibilisi) kuasi, Mungu na Utatu wake Mtakatifu waliamua kumfanya/kumuumba mtu kwa mfano wao. Mtu ambaye walimuumba kwa mfano wao; ambaye ana roho, nafsi na mwili.
Mwanzo 1:26 “Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu…”. Katika mstari huo wa kitabu kitakatifu cha Mungu, Biblia tunaona kuwa Mungu alikuwa akifanya makubaliano na mtu au watu zaidi ya mmoja juu ya kumuumba mtu au mwanadamu. Na aliokuwa akifanya nao maamuzi ya uumbaji wa mtu ni nafsi zake mbili, yaani Mungu mwana (Yesu Kristo) na Mungu Roho Mtakatifu. Mungu katika Utatu wake Mtakatifu ndiye aliye amua kumuumba mtu au mwanadamu kwa ajili ya utukufu wake, na mwanadamu huyu aliumbwa kwa makusudi maalumu ya Mungu mwenyewe.
Inaaminika kwamba Lucifer (ibilisi) alikuwa miongoni mwa malaika wakuu watatu wa Mungu, wengine wakiwa ni Malaika Gabrieli na Malaika Mikaeli amabaye ni malaika wa vita. Wakati ule Lucifer (ibilisi) alikuwa ni malaika mkuu wa sifa, ambaye alikuwa akimpa Mungu utukufu kwa jinsi ya maumbile yake.
Katika ufalme wa Mungu, muundo wa uongozi wa Mungu ulikuwa hivi; Utatu Mtakatifu wa Mungu ndiyo ulikuwa mkuu ukifuatiwa na Malaika hao Wakuu watatu (Lucifer, Gabriel na Michael) na hatimaye walifuatia malaika wengine.
Lakini Lucifer (ibilisi) alipokubali kumuasi Mungu ili akiinue kiti chake juu zaidi ya kiti cha enzi cha Mungu, akitaka kujipa nafasi ya Mungu ndipo aliponyang’anywa utukufu aliokuwa nao na kutupwa hadi kuzimu amabko anatawala jeshi la malaika wao waliokubali kuungana naye katika kumpindua Mungu. Malaika hao waovu ndiyo wajulikanao kama mapepo hivi leo kutoka ufalme wa giza ambao idadi yao ilikuwa ni theluthi ya malaika waliokuwepo Mbinguni wakati ule.
“Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti change juu kuliko nyota za Mungu; name nitaketi juu ya mlima wa mkutano, katika pande za mwisho za kaskazini. Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana nay eye Aliye juu. Lakini utashushwa mpaka kuzimu, mpaka pande za mwisho za shimo” Isaya 14:13-15.
“Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama” Ezekieli 28:17
Mistari ya Biblia hiyo hapo juu unatuonesha jinsi Lucifer ajulikanae kama ibilisi au shetani baada ya kutupwa kuzimu jinsi alivyoasi na kutwa hadi kuzimu. Na kutupwa kwa ibilisi kuzimu haikuwa jambo rahisi, kwani kulitokea vita kati yake na wafuasi wake dhidi ya jeshi la Malaika wa Mungu wakiongozwa na Malaika wa vita Mikaeli.
“Na mkia wake wakokota theluthi ya nyota za mbinguni, na kuziangusha katika nchi.” Ufunuo 12:4(a). katika Biblia, kitabu hicho cha Ufunuo wa Yohana tunaoneshwa idadi ya malaika walioasi pamoja na ibilisi, ambao kwa lugha ya ufunuo wamefananishwa na nyota.
“Kulikuwa na vita mbinguni, Mikaeli na malaika zake wakapigana na yule joka, yule joka naye akapigana pamoja nao na malaika zake; nao hawakushinda, wala mahali pao hapakuonekana tena mbinguni. Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye ibilisi na shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi na malaika zake wakatupwa pamoja naye” Ufunuo 12:7-9.
Baada ya kutupwa hata kuzimu, shetani na malaika zake ambao kwa sasa ndiyo mapepo wakaamua kutengeneza ufalme wao ujulikanao kama ‘ufalme wa giza’ ambao unafanya kazi kinyume na “Ufalme wa Mungu”, ufalme huo wa giza ndiyo uafalme uletao mateso hapa duniani; magonjwa, vita na hali ngumu ya uchumi na mengine yafananayo na hayo. Ashukuriwe Mungu aliyetupa damu ya Mwana Kondoo (Yesu Kristo) ambayo kwa hiyo tunamshinda shetani na ufalme wake wa giza. Na ili kumshinda ni lazima kujikana, na kujikana kwenyewe ni kuamua kumpokea Yesu Kristo kuwa mwokozi wako na kuishi maisha ya utakatifu.
“Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao… Ufunuo 12:11”. Mstari huo wa kitabu kitakatifu, Biblia unatufundisha ni jinsi gani tunaweza kumshinda shetani na ufalme wake wa giza.
Baada ya shetani na ibilisi kutupwa kuzimu, ndipo Utatu Mtakatifu wa Mungu ulipoazimia kumuumba mwanadamu. Na ile nafasi aliyokuwa nayo sheteni katika uongozi wa Ufalme wa Mungu akakabidhiwa mwanadamu huyo. Yaani ngazi ya pili ya ukuu; baada ya Utatu Mtakatifu wa Mungu ndipo mwanadamu huyo anchukua nafasi akifuatiwa na malaika. Na ieleweke kwamba si kila mwanadamu anachukua nafasi hiyo, isipokuwa ni yule tu aliyekubari kuishi kwa kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Ni mwanadamu au mtu yoyote aliye na Ufalme wa Mungu ndani yake. “Na alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza…., Ufalme wa Mungu umo ndani yenu. Luka 17:20-21”. Na hili ni moja ya majukumu au makusudi ya Mungu kumuumba mwanadamu, ili Ufalme wake uwakilishwe hapa duniani kama Mbinguni. Na mwanadamu aliyemkamilifu mbele za Mungu ndiye anayeuwakilisha Ufalme wa Mungu hapa duniani.
“Nami nikaanguka mbele ya miguu yake, ili nimsujudie; akaniambia, Angalia, usifanye hivi; mimi ni mjoli wako na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Msujudie Mungu. Kwa maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii. Ufunuo 19:10”. Huyo aliyetaka kusujudu ni Yohana Mtakatifu, na aliyetaka kumsujudia ni malaika aliyekuwa akimuonesha maono ya Mbinguni. Malaika yule akamwambia ‘usifanye hivyo, mimi ni mjoli wako’, maana yake yeye (malaika) ni mdogo kwake. Na aliposema ‘na wa ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu’, alimaanisha na kila mwanadamu aliyempokea Yesu Kristo kuwa mwokozi wake.
“Haleluya. Msifuni Mungu katika patakatifu pake; Msifuni katika anga la uweza wake. Msifuni kwa matendo yake makuu; msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake. Msifuni kwa mvumo wa baragumu; msifuni kwa kinanda na kinubi; msifuni kwa matari na kucheza; msifuni kwa zeze na filimbi; msifuni kwa matoazi yaliayo; msifuni kwa matoazi yavumayo sana. Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana. Haleluya.” Zaburi 150.
Hiyo ni sababu nyingine au makusudi ya Mungu kumuumba mwanadamu au kumfanya mtu kwa mfano wake, mwanadamu huyu ampe Mungu sifa anazo stahili kutoka na matendo yakemakuu yenye utukufu. Hivyo basi watu wote na tumwimbie Mungu nyimbo za sifa na kutamka sifa midomoni mwetu kwa ajili ya Mungu wetu.

Saturday, September 1, 2012

AMRI KUU


  Mathayo 22:37-38 “…Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu tena ni ya kwanza.”
Katika Biblia habari hii inaanza baada ya Yesu Kristo kuulizwa swali la kujaribiwa na mmoja katika Mafarisayo, ambao walikuwa wanaijua torati kamili ya manabii kwa habari ya sheria na amri zake. Walimuuliza swali wakimjaribu ili awaambie ni amri ipi iliyokuu katika torati, na ndipo Bwana Yesu akawapa jibu tofauti na walilolitegemea. Akawaambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote. Kibinadamu jibu hili ni kama halina mantiki yoyote na limekaa kimzaha zaidi, kwani hakuna mtu asiyempenda Mungu wake.
Lakini ukitazama kiundani zaidi, na kama utapata msaada wa Roho Mtakatifu utagundua kuwa jibu hili linatuhusu na kugusa imani zetu moja kwa moja na siyo wale Mafarisayo tu. Labda tuangalie na kuchambua maana ya vipengere vikubwa vitatu katika mstari wa 37 wa kitabu hicho cha injili.
Kwa moyo wako wote. Neno kwa moyo wako wote linamaanisha kukipa sehemu yote ya moyo wako kitu unachokipenda. Kama umeamua kukipenda kitu fulani, basi ukipende kwa kumaanisha, usikichanganye na kitu kingine. Wala usiwe na mbadala wa hicho unachokipenda.
Kwa roho yako yote, ni kuamua kujitoa hata maisha yako kwa ajili ya hicho unacho kipenda. Kutokuyathamini maisha yako zaidi ya unachokipenda. Sehemu nyingine neno la Mungu linasema atakaye kunifuata na ajikane mwenyewe, sasa kumpenda Mungu kwa roho yote ni kujikana nafsi yako.
Kwa akili zako zote, ni kumfanya Mungu achukue sehemu kubwa ya mawazo yako pasipo kujari sehemu ama wakati uliopo. Kuna watu wakiwa na wapendwa nao ni wapendwa, wakiwa mbali na wapendwa basin a upendwa wao wanauvua.
Kuamua kumpenda Mungu kwa moyo wote, na roho yote, na akili zote, ni kumpenda Mungu pasipo kumchanganya na dhambi, kumpenda Mungu kwa kujikana nafsi zetu na kumpenda Mungu kwa mawazo yetu.
Kuna watu wanawapenda wanandoa wao zaidi ya kumpenda Mungu, wanawapa sifa zinazozidi uzuri wa malaika lakini watu hao hao ukiwakuta kwenye nyumba za ibada wakati wa kipindi cha kumsifu Mungu unawedha ukadhani ni wagonjwa. Na wapo watu wanaowapenda wanadamu kwa roho zao zote kiasi cha kuzirai wakipewa taarifa za vifo vyao lakini kumpenda Mungu hakumo ndani yao. Na wapo watu ambao wanajikana nafsi zao kwa ajili ya watu wengine au mambo mengine. Watu hawa watakwambia hawana muda wa kuhudhuria nyumba za ibada kwa kisingizio cha maisha yanabana au shule ngumu lakini ni mabingwa wa kutenga muda wa kwenda klabu na kumbi mbali mbali za starehe na marafiki lakini muda wa kuongea na Mungu wao hawana.
Kuna aina ya maisha ambayo ni kusudi la shetani moja kwa moja, kama kutoa muda wako mwingi katika vipindi vya televisheni, kusoma vitabu vya hadithi na magazeti, kufanya kazi hadi za “over time”. Lakini linapofika suala la kujitoa kwa Mungu anaye kupa uhai bure, unajibu uko “busy”, hata kusoma biblia yako ni hadi jumapili kanisani, na usomaji wenyewe ni ule wa kufuatisha neno la mhubiri wa siku hiyo.
Hatuna budi kuyatafakari maisha tunayo ishi kuwa ni maisha ya namna ama aina gani, je tunampa Mungu kipaumbele anachostahili katika maisha yetu ya kila siku? Mpenzi msomaji, hebu jiulize swali hilo je mfumo wako wa maisha unampa Mungu kipaumbele anachostahili? Na kama jibu ni ndiyo basi Mungu akuzidishe zaidi, na ikiwa jibu ni siyo basi Mungu akusaidie ili umpe nafsi yake anayostahili katika maisha yako.
Kama tunavyo oona katika mstari ule wa 38 wa injili hii, Yesu aliwajibu wale Mafarisayo kuwa amri hii ndiyo kuu tena ni ya kwanza. Kuvunja amri kuu ni kutenda kosa kuu.

Saturday, August 25, 2012

SENSA


  Luka 2:1-5 “… Yusufu naye aliondoka Galilaya, toka mji wa Nazareti, akapanda kwenda Uyahudi mpaka mji wa Daudi, uitwao Bethlehemu, kwa kuwa yeye ni wa mbali na jamaa ya Daudi; ili aandikwe pamoja na Mariamu mkewe, ambaye amemposa, naye ana mimba”.  
Ukisoma kwa makini katika mistari ya injili hiyo hapo juu kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka; neno linatuambia kuwa Yusufu alifunga safari yeye pamoja na Mariamu mkewe ambaye alikuwa mjamzito (mwenye ujauzito wa Bwana wetu Yesu Kristo) kutoka mji aliokuwa anaishi wa Nazareti ulioko Galilaya na kwenda katika mji wa Daudi yaani Bethlehemu ulioko Uyahudi. Kilichomfanya afanye safari ile ni amri iliyotolewa na Kaisari Augusto, iandikwe orodha ya majina ya watu wotewa ulimwengu (ambayo ilikuwa ni orodha ya kwanza kuandikwa hapo Kirenio).
  Hiyo ilikuwa ni sensa inayofanana na hii tunayoifanya wananchi wa Tanzania kwa mujibu wa katiba kila baada ya miaka kumi, ili kuijua idadi yetu na hivyo kuipa urahisi serikali yetu katika mipango yake ya maendeleo kwa sekta mbali mbali za kijamii kama afya, elimu, miundombinu n.k. Kuna baadhi ya wenzetu wamekuwa wakiihususha shughuli hii na ushirikina na wapo ambao wamekuwa wakiipinga kwa sababu zao binafsi aidha za kimaslahi au kisiasa. Kwa mkristo yoyote kukataa kuhesabiwa kwa kujishawishi yeye mwenyewe au kwa ushawishi wa mtu mwengine yoyote ni kwenda kinyume na neno la Mungu na hivyo ni kosa kama kuivunja amri yoyote ya Mungu, kama biblia inatuonesha Yusufu na mkewe Mariamu walihesabiwa na wewe hutaki kuhesabiwa ni kosa.

Sunday, August 19, 2012

MIMI NDIMI BWANA NIKUPONYAYE


  Kutoka 15:26 “…kwa kuwa Mimi ndimi Bwana nikuponyaye.” Watu wengi wamekuwa wakihangaika kwenda huku na huko wakitafuta uponyaji wa magonjwa na madhaifu ya namna mbali mbali yanayowasumbua katika afya za miili yao, inawezekana ukawa wewe au ndugu yako wa karibu. Na mara nyingine utawakuta watu wa namna hii wamefikia hata hatua ya kwenda kwa waganga wa kienyeji. Ngoja nikufungue akili utambue kitu; ili mtu awe daktari ni lazima afundishwe na madaktari masomo yanayohusu udaktari, na ili mtu awe mganga wa kienyeji ni lazima afundishwe uganga wa kienyeji na mganga wa kienyeji. Na ukikuta mganga wa kienyeji anasema ngoja tuiulize mizimu ama kwa lugha nyingine wanawaita waungwana utambue moja kwa moja kuwa uganga wake una mahusiano na nguvu za giza (uchawi). Ni vema kutumia chakula; mboga za majani na matunda kwa kujenga na kulinda afya yako na hata kutibu baadhi ya magonjwa kama masomo yapatikanayo katika ukurasa wa dondoo za afya (Health Tips)  yanavyokuelekeza.
  Napenda nikwambie kama jinsi Mungu anvyosema, “Mimi ndimi Bwana nikuponyaye” anamaanisha anachokisema na kamwe Mungu hajawahi na hatawahi kusema uongo. Hebu tuangalie ahadi nyingine za neno la Mungu kuhusu kutuponya na magonjwa na madhaifu yanayotupata:-

Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts