Ufunuo wa Yohana 21:5
...tazama, nayafanya yote kuwa mapya...
Bwana Yesu asifiwe!
Ninakusalimu kupitia Jina la Yesu Kristo mpendwa msomaji wangu.
Kuna swali napenda ujiulize mpendwa msomaji wangu, leo nakwenda kuongea na mtu mmoja au nafsi moja, naongea na wewe!
SWALI; Licha ya neema, baraka, ulinzi na mema yote Mungu anayokutendea katika maisha yako (Yeremia 29:11-12), kwanini unatenda au unadhamiria kutenda dhambi???
Inawezekana wewe siyo mtu sahihi kwa swali hili, lakini yupo mtu sahihi ambaye ujumbe huu utakwenda kumponya na kumfanya kiumbe kipya. Kama wewe ni mtu sahihi kwa swali hili, je umewahi kujiuliza swali hilo hapo juu??? Viongozi wa dini na hata waumini wenzako wanadhani unaendelea vema, kumbe uliisha jitenga na imani kitambo sana, na yupo mpendwa mwingine anajulika kuwa anatenda dhambi na wapendwa wakimkanya anajifanya kuomba ushahidi, nikuulize swali, umewahi kwenda mbele za Mungu na kumwambia akupe ushahidi wa uovu wako? Najua huwezi kufanya hivyo kwa sababu Mungu hadhihakiwi na hadanganywi na jambo!
Kwa maana hiyo, hauwadanganyi viongozi wako wa dini na wapendwa, haujifichi mbele zao, hauwezi pia kumdanganya au kujificha mbele za Mungu, BALI unaidanganya nafsi yako. Kwanini kujidanganya nafsi basi???
JIBU; ...mungu wa dunia hii (ibilisi/shetani) amepofusha fikira zao, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo...(2 Kor 4:4)
Hakuna mwanadamu atendaye dhambi kwa matakwa yake binafsi, isipokuwa ametiwa upofu nafsini na ndani ya nia yake na ibilisi asione aibu ya dhambi. Kutenda dhambi ni aibu, tena nasema ni aibu, kama ilivyo kwa timamu kutembea bila nguo. Na hii ndiyo sababu dhambi hutendwa kwa kificho, gizani kwani anayepofusha na kumfanya mwanadamu atende dhambi ni mfalme wa giza, shetani au ibilisi. Na mtenda dhambi hutenda dhambi kwa kutimiza matakwa ya ibilisi/shetani...yaani, shetani hutumia mwili wa mwanadamu kutenda dhambi au kufanya uovu; kufanya uzinzi, uasherati, uuaji, wizi, tamaa mbaya iletayo mauti n.k (Waefeso 2:1-2)
Mpenzi msomaji wangu, sihukumu nafsi ya mtu kwa maana sipo katika nafasi ya kuhukumu, mwenye kuhukumu na kurehemu/kusamehe dhambi ni Mungu peke yake kupitia Kristo Yesu. Leo Mungu amekuona, kupitia damu ya Yesu Kristo atakwenda kukusamehe na kukutakasa kabisa.