Friday, April 27, 2018

IMARISHA MAHUSIANO YAKO YA NDOA NA MAHUSIANO YAKO NA MUNGU


Mpendwa msomaji, ninakusalimu kupitia Jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Nina habari njema kwako zenye baraka kutoka kwa Mungu. Neno la Mungu linatuagiza waamini kutomuacha elimu aende zake. Nini basi makusudi ya agizo hilo? Hakuna muamini anayeweza kukua na kuimarisha uelewa na ufahamu wake kwa habari ya elimu ya dunia na elimu ya Mungu pasipo kuwa na mpango madhubuti wa kuitafuta na kuikamata elimu hiyo. 

Huwezi kumtumikia Mungu ipasavyo kama hauna elimu ya kutosha kumuhusu. Na kama haumtumikii Mungu inavyostahili, hauwezi kukua kiroho kwa viwango vya utakatifu vinavyohitajika. Vivyo hivyo, hauwezi kuandaa ndoa yenye upendo imara (wanaotarajia kufunga ndoa) au kuwa na ndoa imara iliyojaa upendo, kujali na kuthamini kama hautakuwa na elimu kuhusu ndoa kwa mujibu wa Biblia takatifu. Hauwezi kuimarisha mahusiano yako ya ndoa au mahusiano yako na Mungu kupitia maombi peke yake, ni lazima usome. 

Habari njema ninazokuletea leo ni tarajia vitabu vizuri vyenye uwepo wa Mungu na uvuvio wa nguvu za Roho Mtakatifu kwa Jina la Yesu Kristo.

Kitabu cha kwanza kinaitwa, “THE HAPPIEST EVERLASTING MARRIAGE, Principles for Happiest Marriage”.  Ndani ya kitabu hiki utajifunza namna ipasayo ili kuwa na mahusiano ya ndoa imara kuanzia uchumba hadi malezi bora ya watoto kwa kadiri utakavyo barikiwa na Mungu. Kila mmoja anakihitaji kitabu hiki, siyo wana ndoa peke yao, hata vijana wanaotarajia kufunga ndoa miaka michache ijayo.

Kitabu cha pili kinaitwa, “EFFECTIVE TALKING WITH GOD, Becoming God’s Friend”.  Katika kitabu hiki utajifunza kukuza imani yako na uhusiano wako na Mungu, namna sahihi ya kujihudhurisha mbele za Mungu na kufikia viwango vya kuwa rafiki wa Mungu. 

Vitabu hivi bado havijawa tayari kwa sasa, vipo katika hatua ya “peer reviewing” ili kuhakiki ubora wake. Miezi michache ijayo, vitabu vyote vitakuwa vinapatikana sokoni na vitauzwa na wauzaji wa kimataifa kwa njia ya mtandao kama Amazon.com. Vitabu vyote vimeandikwa kwa lugha ya Kiingereza ili kuvipa wigo mkubwa zaidi wa wasomaji kwa Jina la Yesu Kristo. 

Usipange kuvikosa vitabu hivi, na Mungu atakubariki sana. Amina.

Monday, April 16, 2018

TUNAOWAPENDA SANA NDIYO WANAOTUUMIZA SANA: NAMNA YA KUYASHINDA MAUMIVU HAYO


Nakusalimu kupitia jina la Mwalimu Mkuu, Yesu Kristo.

Binti wa umri wa miaka 5 alitenda kosa mara moja, mama yake akamchapa viboko vitatu huku akimkanya kwamba alichofanya ni kosa asilotakiwa kulirudia tena, yule binti mdogo alilia akisema, “mama nimekosa, sitarudia tena”. Kwa mara nyingine yule binti mdogo alikosea tena, siku hii baba alikuwa nyumbani, binti yule kipenzi cha baba alipokosea. Baba akamchapa binti yake kiboko kimoja na kumkanya kutorudia tena kosa lile. Yule binti mdogo alilia sana, kwa uchungu na hakutaka kubembelezwa na mtu yoyote yule isipokuwa baba yake aliyemchapa.
Katika simulizi hiyo hapo juu tunajifunza mambo makuu mawili. Mosi; binti mdogo alilia zaidi alipochapwa kiboko kimoja na baba kuliko alipochapwa viboko vitatu na mama. Hii ni sababu yule binti mdogo ni kipenzi cha baba zaidi ya mama. Alipochapwa na mama hakujali sana, aliona anafundishwa kutokosea. Lakini alipochapwa na baba aliona ameonewa, kwa upendo mkubwa wa dhati baina yake na baba yake, haikupaswa baba amuadhibu kwa kukosea kwake. Pili; binti mdogo hakutaka kubembelezwa na mtu yoyote isipokuwa baba yake aliyemuadhibu kwa sababu, kubembelezwa na baba ni sawa na baba kuomba msamaha kwa kumuadhibu binti yake, jambo ambalo lingempa faraja binti mdogo yule.
Wanadamu wote tuna tabia inayofanana na huyu binti mdogo katika simulizi hii, hivyi ndivyo tulivyoumbwa tangu utoto wetu. Tukikosewa au kutendwa na tunaowapenda sana, tunaumia sana mioyoni mwetu na kubeba maumivu ambayo hudumu mioyoni mwetu kwa muda mrefu sana kuliko tukikosewa na watu wasio karibu nasi au wapendwa kwetu. Uchungu hujaa mioyo yetu kwa sababu hatutegemei wale tunaowapenda sana kutuumiza, tunajizuia sana kutowaumiza ili tusiwapoteze, tunategemea nao wafanye sawa na hivyo. Hatuwezi kutua mzugo wa uchungu uliojaza mioyo yetu hadi pale tutakapo sikia neno la kuomba msamaha kutoka kwa waliotuumiza. Kila siku unatamani na kusubiri aliyekuumiza akwambie samahani, pole, sitakuumiza tena. Nafsi yako ipate furaha na amani.
Kuna watu wamefanya maamuzi magumu, hata kujiumiza zaidi katika miili yao au kujitoa uhai kwa sababu ya kushindwa kuvumilia na kuyashinda maumivu yaliyosababishwa na wanaowapenda sana. Katika somo hili utajifunza kupokea maumivu kutoka mtu yoyote na namna ya kuyakabili maumivu hayo ili kuepuka madhara yanayoweza kusababishwa na maumivu hayo ikiwemo kuchanganyikiwa akili au kujitoa uhai.

Mtu yoyote anaweza kukuumiza nafsi
Tunawaamini sana wanadamu wenzetu, kiasi kwamba hatudhani kama wanaweza kutusababishia maumivu makubwa na yenye madhara kwetu. Tunadhani, endapo tutawatendea wema nao wataturudishia wema na kumbe sivyo, wanaweza kutulipa ubaya wenye kuumiza zaidi. Kuna mtu alisema, “wewe kutomla simba haimaanishi simba kutokukula wewe” au “not eating a lion doesn’t mean a lion won’t eat you”. Kutowatendea mabaya tunaowapenda haimaanishi wao pia hawatatutendea sisi mabaya katika hatua moja au nyingine ya maisha yao. Ukweli huu ndio unaotufanya tuumizwe sana endapo tunaowapenda watatutenda ubaya, kwa sababu hatutegemei kupokea mabaya kutoka kwao. Kuna watu wameumizwa hata wakasema hawata samehe kamwe kwa sababu tu waliowaumiza ni waliowapenda zaidi. Kusamehe ni lazima. Ufundishe moyo wako kutegemea chochote; ubaya au wema kutoka kwa yoyote. Anayetuwazia na kutupatia mema siku zote za uhai wetu ni Mungu pekee.

Mara baada ya kuumizwa na uliyempenda sana, samehe kwa dhati
Hakuna mwanadamu aliyemkamilifu kwa namna moja au nyingine, sote tuna mapungufu isipokuwa Mungu pekee. Katika maisha yetu ya kila siku, mtu mmoja anaweza kummumiza mtu mwingine kwa kutokukusudia au kwa kukusudia. Baada ya kusababisha maumivu anaweza kuomba msamaha au hata asiombe msamaha tena kwa makusudi hasa kama akitambua aliyekuumiza huwezi kumuumiza kwa kulipa kisasi (makusudi) au bahati mbaya. Uambie moyo wako usamehe na kuachilia mzigo wa hasira na maumivu uliyoyabeba. Tunaposamehe ni kwa faida yetu kwanza, Waefeso 4:31-32 na Mathayo 6:14-15 (tunajiponya nafsi na kupata kibali cha msahama mbele za Mungu) na faida ya tunaowasamehe. Ndio, faida ya tunaowasamehe. Wapo wasioweza (wanaokosa ujasiri) kuomba msamaha kwa sababu wao pia huumia mara baada ya kuona wamewaumiza wanaowapenda sana.

Usitake kujua sababu ya kuumizwa kwako
Wanadamu wengi tunapenda kujua sababu ya kuumizwa kwetu tukidhani itasaidia kutoumizwa tena. Lakini nikufahamishe, wengi wanaotuumiza huwa hawana sababu madhubuti za kutuumiza, na endapo tutahitaji kujua sababu, hawataweza kutupatia sababu madhubuti vile vile. Hivyo, siyo muhimu kujua sababu ya kuumizwa zaidi ya kusamehe na kuachilia.

Usilipe kisasi
Usiwe na tabia ya kulipa kisasi kwa waliokutendea ubaya. Kulipa kisasi ni kuumia zaidi, hasa utakapotambua aliyekuumiza hakukusudia kufanya hivyo. Nafsi yako itakuwa imeumia mara mbili kwa kuiumiza nafsi isiyo na hatia. Moyo wako utajaa chuki na hasira dhidi yako binafsi. Hasira au chuki binafsi “self denial” ina madhara makubwa sana. Idadi kubwa ya wanadamu wanojitoa uhai wanakuwa chini ya utawala wa hii roho chafu “self denial”. Mungu anatuagiza tusilipe kisasi, kwa sababu kisasi ni chake (Warumi 12:19 na Mithali 24:29) na siyo chetu.

Waombee na kuwapenda wanaokutenda ubaya
Hili ni agizo la Mungu (1 Petro 3:9), tuwaombee na kuwapenda wanaotutenda ubaya. Hii ni kwa sabau kubwa mbili, moja; Mungu hutubariki na kutuinua na pili; huwafanya waliotutenda ubaya kujifunza wema wa Mungu kupitia maisha yetu. Tunapowaombea waliotuudhi tunainuliwa kiimani, waombe heri na siyo laana. Pia Mungu huachilia baraka zake kwetu maradufu zaidi ya tuombavyo, kwa sababu huonesha roho, moyo na nafsi iliyopondeka na kunyenyekea mbele za Mungu zaidi ya maumivu tuliyonayo mioyoni. Tunapowalipa mema waliotutenda ubaya, inawapa fundisho la kuuona wema wa Mungu kupitia maisha yetu. Inakufanya ufanyike baraka kwa wote, wema na waovu kwako, hii ni tabia halisi ya Mungu, huwanyeshea mvua wema na waovu.

Dumu katika sala na maombi, ni nguzo madhubuti ya kuishi maisha yenye amani, furaha na upendo. Amina.

Tuesday, February 20, 2018

MPANGO KAZI WA KIBIBLIA WA KUTATUA CHANGAMOTO ZA MAISHA

Nakusalimu mpenzi msomaji wangu, Jina la Yesu Kristo lisifiwe.

Leo napenda kuanza na hadithi kwa ufupi sana,
Ninaishi katika jamii ya wafugaji ambao hutegemea malisho ya mifugo yao; ng’ombe, mbuzi na kondoo katika majani yaotayo kondeni na vichakani. Wengi wa wafugaji hawa wanamiliki idadi kubwa ya mifugo, hivyo huwalazimu kutoka na mifugo yao kila siku kwenda kutafuta malisho na maji. Vijana wa kiume wa umri wa kati, huamka mapema asubuhi, hutoa mifugo katika mazizi yao, huiswaga na kuiongoza mifugo hii sehemu yalipo malisho mazuri na maji. Kila ifikapo jioni, hufanya kama walivyofanya asubuhi, huiswaga na kuiongoza mifugo yao kuirudisha mazizini mwao. Wafugaji hawa wanaotembea na mifugo yao kwa lengo la kutafuta malisho na maji huitwa wachungaji.

Wachungaji hawa hukaa nyuma na kuitanguliza mifugo yao mbele kwa lengo la kuweza kuiangalia isitawanyike na kufanya uharibifu wa mazao na mazingira wawapo njiani kuelekea malishoni ama kurudi mazizini. Katika kundi la mifugo isiyopungua hamsini, mifugo iliyotangulia mbele huchoka kutokana na safari ya mwendo mrefu kwenda na kurudi kutafuta malisho, hivyo hupunguza mwendo kasi wa kutembea. Mifugo iliyotangulia mbele ikipunguza mwende kasi wa kutembea, huilazimu mifugo yote inayofuata pamoja na mchungaji kupunguza mwendo kasi. Mara tu mwendo kasi wa kutembea unapopungua mchungaji huichapa mifugo iliyo karibu naye, mifugo ya nyuma, ili iweze kuongeza mwendo pasipo kujali kuwa mifugo iliyo mbele ndiyo inayopunguza mwendo hivyo basi mifugo ya mbele ndiyo ilistahili kuchapwa. 

Mifugo ya nyuma iliyochapwa huanza kukimbia na kuisukuma mifugo ya mbele, ambayo hukumbuka, kumbe tumepunguza mwendo, na kuanza kukimbia pia ili kuongeza mwendo. Mifugo ya mbele inajisahau kutunza mwendo kasi, inaanza kutembea taratibu, ili kukumbushwa kuongeza mwendo kasi, inachapwa mifugo ya nyuma ambayo siyo sababu ya kupungua kwa mwendo kasi. Mara baada ya kuchapwa, huikumbusha mifugo ya mbele kuongeza mwendo kasi, na mara mwendo kasi unaongezeka. Hayo ndiyo maisha ya kila siku ya mifugo inayobaki nyuma katika msafara wa kwenda ama kurudi malishoni. Hupokea kipigo kisicho na sababu. 

Tujifunze nini katika hadithi ya leo? Hadithi ya leo inatufundisha mambo makubwa matatu; 1. Changamoto ni lazima 2. Usilalamikie changamoto 3. Kabiliana na changamoto. 

Monday, September 12, 2016

SADAKA

Bwana Yesu asifiwe mpendwa msomaji wetu!

Tunajiandaa kwenda kuwatembelea wazee na walemavu wa ukoma waishio katika nyumba za wazee hapa jijini Mwanza, serikali imefanya sehemu yake ya kuwajengea nyumba za kuishi, na sisi kama kanisa la Mungu kwa umoja wetu tunadhamiria kufanya kwa sehemu yetu kadiri Mungu atakavyotubariki. Tunategemea kuwapelekea mahitaji muhimu kwa maisha kama vile; chakula na mavazi.

Tunajipa muda wa mwezi mmoja tangu sasa (12/09/2016), ifikapo tarehe 12/10/2016 tunatarajia kuwa tumejipanga na kujiandaa vya kutosha.

Tunapenda ushiriki baraka hizi pamoja nasi, vile unavyobarikiwa na jumbe mbali mbali ndani ya "blog" hii, SILAGO2.BLOG na namna unavyomshuhudia Mungu kukutana nawe katika maisha yako na hata kufunguliwa kwa namna moja ama nyingine, tunapenda umshangilie Mungu kwa furaha iliyoambata na sadaka yako ili kuwasaidia wenye uhitaji.

Mungu anasema ikiwa twajisifu tuna dini iliyo safi (dini sahihi), na hatuwatazami wahitaji katika dhiki yao, twajidanganya. Dini iliyo safi ni kuwatazama (kuwasaidia) wahitaji (yatima, wajane, wazee) katika dhiki yao (Yakobo 1:27)

Na utoapo sadaka yako, toa kwa moyo wa kupenda (Zaburi 54:6), pia hakikisha unaisemea jambo sadaka yako kuhusu maisha yako ya kiroho au kimwili kulingana na uhitaji wako (Zaburi 50:5).

Ili kushiriki baraka hizi, unaweza kutuma mchango wako wa fedha kwa M-pesa kupitia namba;
0759 982 604 au kwa kutoa sadaka yako ya mali (siyo fedha) wasiliana nasi HAPA.

Tunakaribisha watu wote pasipo kujali tofauti za imani/dini zetu.

Mungu abarikiye, na atakwenda kukubariki kwa kadiri ya utakavyo toa na imani yako. Amina.

Sunday, September 11, 2016

MWANZO MPYA WA MILELE NDANI YA YESU KRISTO

Ufunuo wa Yohana 21:5
...tazama, nayafanya yote kuwa mapya...

Bwana Yesu asifiwe!
Ninakusalimu kupitia Jina la Yesu Kristo mpendwa msomaji wangu.

Kuna swali napenda ujiulize mpendwa msomaji wangu, leo nakwenda kuongea na mtu mmoja au nafsi moja, naongea na wewe!
SWALI; Licha ya neema, baraka, ulinzi na mema yote Mungu anayokutendea katika maisha yako (Yeremia 29:11-12), kwanini unatenda au unadhamiria kutenda dhambi???
Inawezekana wewe siyo mtu sahihi kwa swali hili, lakini yupo mtu sahihi ambaye ujumbe huu utakwenda kumponya na kumfanya kiumbe kipya. Kama wewe ni mtu sahihi kwa swali hili, je umewahi kujiuliza swali hilo hapo juu??? Viongozi wa dini na hata waumini wenzako wanadhani unaendelea vema, kumbe uliisha jitenga na imani kitambo sana, na yupo mpendwa mwingine anajulika kuwa anatenda dhambi na wapendwa wakimkanya anajifanya kuomba ushahidi, nikuulize swali, umewahi kwenda mbele za Mungu na kumwambia akupe ushahidi wa uovu wako? Najua huwezi kufanya hivyo kwa sababu Mungu hadhihakiwi na hadanganywi na jambo!

Kwa maana hiyo, hauwadanganyi viongozi wako wa dini na wapendwa, haujifichi mbele zao, hauwezi pia kumdanganya au kujificha mbele za Mungu, BALI unaidanganya nafsi yako. Kwanini kujidanganya nafsi basi???

JIBU; ...mungu wa dunia hii (ibilisi/shetani) amepofusha fikira zao, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo...(2 Kor 4:4)
Hakuna mwanadamu atendaye dhambi kwa matakwa yake binafsi, isipokuwa ametiwa upofu nafsini na ndani ya nia yake na ibilisi asione aibu ya dhambi. Kutenda dhambi ni aibu, tena nasema ni aibu, kama ilivyo kwa timamu kutembea bila nguo. Na hii ndiyo sababu dhambi hutendwa kwa kificho, gizani kwani anayepofusha na kumfanya mwanadamu atende dhambi ni mfalme wa giza, shetani au ibilisi. Na mtenda dhambi hutenda dhambi kwa kutimiza matakwa ya ibilisi/shetani...yaani, shetani hutumia mwili wa mwanadamu kutenda dhambi au kufanya uovu; kufanya uzinzi, uasherati, uuaji, wizi, tamaa mbaya iletayo mauti n.k (Waefeso 2:1-2)

Mpenzi msomaji wangu, sihukumu nafsi ya mtu kwa maana sipo katika nafasi ya kuhukumu, mwenye kuhukumu na kurehemu/kusamehe dhambi ni Mungu peke yake kupitia Kristo Yesu. Leo Mungu amekuona, kupitia damu ya Yesu Kristo atakwenda kukusamehe na kukutakasa kabisa.

Wednesday, August 31, 2016

SALAMU KATIKA KRISTO YESU, BWANA WETU

Bwana Yesu asifiwe, mpendwa msomaji wetu!
Tunakusalimu kupitia Jina la Yesu Kristo, Jina liponyalo na liokoalo. Amina.

Tunapenda kuwajulisha wasomaji wetu wote kuwa, baada ya kimya cha miaka takribani miwili sasa tunarudi tena hewani kwa nguvu mpya katika Jina la Yesu Kristo. Tegemea kubarikiwa, kukutana na Mungu na hata kupokea uponyaji kwani Yesu Kristo tumuaminiye hashindwi na jambo ikiwa imani yetu haiteteleki.

Jiandae na somo lenye kichwa, "MWANZO MPYA WA MILELE NDANI YA YESU KRISTO". Ni somo litakalokwenda kuimalisha maisha yako ya kiroho na kuinua imani yako zaidi kwa utukufu wa Mungu mwenyewe. Usikose!!!

Mungu wa mbinguni aishiye milele, akubariki sana. Amina.

Wednesday, December 24, 2014

HERI YA KRISMASI NA FURAHA YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO, 2015

 Uongozi wa blogu ya "SILAGO2.BLOG", wachungaji walezi na wapendwa katika pendo liokoalo la Yesu Kristo, tunawatakia wasomaji wetu wote mahali popote mlipo "HERI YA KRISMASI NA FURAHA YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO, 2015".

Kwanza kabisa tunazo shukurani za dhati kwa Mungu aliye hai, aishiye milele, Yehova kupitia Jina la Yesu Kristo kwa kuwa nasi tangu kuanza mwaka wa 2014. Kwa uaminifu, neema na rehema zake ametuvusha salama na kwa imani tutauona mwaka wa 2015. Inawezekana umepoteza wapendwa wako, lakini huna budi kumshukuru na kumtukuza Mungu kwa neema na fadhili zake nyingi alizokutendea.

Pili, tunawashukuru wasomaji na wapenzi wetu wote kwa sababu uwepo wenu ndiyo uwepo wa blogu hii. Mungu wa mbinguni, Yehova awabariki wote na kuwajalizia haja za mioyo yenu kupitia Jina lipitalo majina yote la Yesu Kristo, Amina.

Tatu, tungependa kuwakumbusha kuwa siku kuu za Krismasi na Mwaka mpya zina maana tofauti na jinsi tunavyo zisherehekea. Krismasi ni siku ya kuzaliwa kwa Mfalme, mkombozi wa wanadamu kutoka utumwa wa shetani. hivyo basi, itumie siku hii kuutafakari upendo mkuu wa Mungu na Yesu Kristo kwako, na ukubali kujiachilia moyo wako wazi mbele za Mungu ili "Utatu mtakatifu wa Mungu" uingie na kuishi nawe.
Mwaka mpya ni siku kuu inayotukumbusha neema na rehema za Mungu kwetu, kwamba katika mwaka unaoisha kuna makosa tulimkosea Mungu, lakini bado kwa upendo wake ametuzawadia uzima na afya ambavyo hatukuvistahili kwa kuenenda kwetu katika kutimiza tamaa za miili yetu. Hivyo basi, hatuna budi kutubu, kutengeneza tena uhusiano mzuri na Mungu wetu kupitia damu iokoayo ya Yesu Kristo.

Katika kipindi hiki kifupi cha siku kuu za Krismasi na Mwaka mpya weka historia nzuri ya ushindi, tumia kipindi hiki kujenga umoja, ukaribu na mshikamano, mkiongeza chachu ya upendo na furaha katika familia. Kwa sababu familia yenye amani, furaha na upendo ndiyo familia yenye mafanikio ya kiroho na kimwili.

"KHERI YA KRISMASI NA FURAHA YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO, 2015"


Featured Post

HAIJALISHI TUNAKOSEA MARA NGAPI? MUNGU NI MUAMINIFU KILA WAKATI

Nakusalimu kupitia Jina kuu lipitalo majina yote, Jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu. Mungu wetu ni muaminifu, hajawahi kuse...

Popular Posts